Sura ya Qaaf, aya ya 16-22 (Darsa ya 950)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 950 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 50 ya Qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya yake ya 16 ambayo inasema:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ
Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua inayomtilia wasiwasi nafsi yake. Na Sisi tukaribu naye zaidi kuliko mshipa wa shingo (yake).
Katika darsa iliyopita tulieleza kwamba, maudhui kuu ya Suratu Qaaf ni kuhusu Kiyama. Aya hii tuliyosoma inazungumzia elimu na ujuzi wa Allah SWT juu ya amali na matendo ya mwanadamu na kueleza kwamba, Yeye Mola ndiye Muumba wa mwanadamu na ana ujuzi kamili wa kila kitu cha ujudi wa kiumbe huyo na hali zake zote. Allah SWT sio mjuzi tu na mwenye habari za mambo yote ayafanyayo mtu, bali ni mtambuzi pia wa yote anayoyawaza na kuyafikiri na kila kinachompitikia kiumbe huyo akilini mwake. Pamoja na hayo, kwa rehma na uraufu alionao kwa mja wake, Yeye Mola huwa hamuadhibu mtu kwa sababu ya wasiwasi na fikra mbaya na chafu zinazompitikia akilini mwake; tab'an ikiwa hatafikia hatua ya kutenda tendo baya. Uhai wa mtu umefungamana na mishipa mbalimbali iliyoungana na moyo, ambao hufanya kazi ya kusambaza damu kupitia mishipa hiyo hadi kwenye viungo tofauti vya mwili; na tab'an Mwenyezi Mungu TWT yu karibu zaidi na mtu kuliko hata hiyo mishipa ya kiwiliwili chake. Na sababu ni kuwa uhai wa mwanadamu, kwa hakika uko mikononi mwa Allah; na moyo na mishipa yote hiyo ya kiumbe huyo ni wenzo tu wa kutekelezea irada na yaliyokadiriwa na Mola. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hii ni kwamba, ujuzi na uwezo wa Mwenyezi Mungu Jalla Jalaaluh hauna kikomo wala mpaka; na umemzunguka kikamilifu mwanadamu, tena muda wote. Uelewa na utambuzi wa Allah juu ya hali na mambo ya mwanadamu ni mpana na makini mno. Kwa hivyo kama tunadhani Yeye Mola hayajui tunayowaza, tunayoyapanga na tunayoyadhamiria ndani ya nafsi zetu, basi dhana yetu hiyo ni batili na potofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama hatutazichunga nafsi zetu, basi kwa kupitia njia tofauti, zitatuchochea na kutujaza wasiwasi mtawalia wa kufanya mambo yasiyofaa mpaka ihakikishe tunateleza na kuharibikiwa.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 17 na 18 ambazo zinasema:
إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ
Wanapo pokea wapokeaji wawili, walioko kuliani na kushotoni.
مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ
Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari (kuandika).
Baada ya aya iliyotangulia kuelezea elimu na ujuzi wa Allah kwa fikra na mawazo yanayopita ndani ya akili ya mtu, aya hizi zinazungumzia kuhifadhiwa kwa mambo yote ayafanyayo mwanadamu na kubainisha kwamba: Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla amemwekea kila mtu malaika wawili wanaomfuatilia na kumchunga muda wote. Malaika hao wananakili na kuandika mambo yake yote mema na mabaya, na hakuna chochote kinachofichika mbele yao. Watu wengi sana huwa hawachukulii maneno wayasemayo kuwa ni sehemu ya amali na matendo yao na kwa hivyo huwa hawajali sana ni kitu gani kinatamkwa na ndimi zao, ilhali kauli na maneno yana nafasi na mchango muhimu katika miamala ya kijamii na kifamilia ya mtu. Na ndiyo maana katika aya hizi, Qur'ani tukufu imezungumzia peke yake maneno yasemwayo na mtu na kueleza kwamba, kila neno litokalo kinywani huandikwa na kuhifadhiwa na malaika hao wawili. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, japokuwa Yeye Allah mwenyewe ni mjuzi wa ya batini na ya dhahiri ya mtu, lakini kila jambo ameliwekea wenzo na sababu za utendaji wake; na ndio maana amewaamuru malaika maalumu kufanya kazi ya kuandika na kuhifadhi matendo na amali zote za mja. Funzo jengine tunalopata katika aya hizi ni kuwa, kuamini kuwepo kwa malaika ni moja ya vielelezo vya imani juu ya ghaibu inayoandamana na kumwamini Allah SWT. Halikadhalika, aya hizi zinatutaka tutambue kwamba, mwanadamu anabeba dhima na masuulia sio tu ya matendo yake, lakini pia ya kila kitamkwacho na ulimi wake, na lolote lile linalotokana na yeye atakwenda kuulizwa na kuhesabiwa kwalo Siku ya Kiyama.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 19 hadi ya 22 za sura yetu ya Qaaf ambazo zinasema:
وَجَاءَتْ سَكْرَةُ الْمَوْتِ بِالْحَقِّ ۖ ذَٰلِكَ مَا كُنتَ مِنْهُ تَحِيدُ
Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia.
وَنُفِخَ فِي الصُّورِ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْوَعِيدِ
Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.
وَجَاءَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّعَهَا سَائِقٌ وَشَهِيدٌ
Na itakuja kila nafsi pamoja nayo mpelekaji na shahidi.
لَّقَدْ كُنتَ فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَٰذَا فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءَكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ
(Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.
Wakati mtu anapofikwa na mauti, hupatwa na hofu na mfadhaiko wa ajabu. Ni kawaida kwa watu wote kujaribu kukihepa kifo na kutopenda hata kufikiria jambo hilo. Na kama watataka kuvuta taswira ya mauti, basi hufanya hivyo kwa kuwaza na kufikiria vifo na mauti ya wenzao. Lakini Qur'ani inasema, mauti ni jambo la haki na yatakufikeni nyinyi nyote, iwe mumejiandaa nayo au la. Pamoja na hayo na bila ya shaka, kifo maana yake si kumalizika na kutoweka moja kwa moja kwa mwanadamu, bali ni kuhamishwa kutoka ulimwengu mmoja kuelekea ulimwengu mwingine, ambako hakuna shaka kuwa kunaandamana na hali ngumu na nzito na kutengana mtu na jamaa na wapendwa wake. Na ndivyo inavyokuwa wakati wa kuzaliwa pia, ambapo mwanadamu huhamishwa kutoka kwenye maisha ya kiinitete kilichomo tumboni kuelekea kwenye maisha ya duniani yanayoandamana na sauti ya kilio ya mtoto mchanga anayekatwa kiungamwana cha kitovu chake. Wakati wa kuzaliwa, huwa tunatoka matumboni mwa mama zetu na kutia mguu juu ya mgongo wa ardhi. Na baada ya mauti, tunarejeshwa kwenye tumbo la ardhi; na wakati wowote atakapotaka Allah, tutatoka kwenye tumbo hilo la ardhi na kutia mguu tena ardhini. Lakini kinyume na mara ya kwanza, mara hiyo ya pili tutarejeshwa ili kwenda kuwajibika kwa kuyatolea majibu matendo na amali zote tulizofanya mara ya kwanza hapa ardhini. Kama ilivyokuwa duniani, Siku ya Kiyama pia malaika wawili wa kila mmoja wetu wataandamana nasi ili kutuhudhurisha mbele ya mahakama ya uadilifu ya Mwenyezi Mungu na watatoa ushahidi juu ya mambo tuliyofanya hapa duniani. Wakati huo ndipo mtu atafahamu na kubaini kwamba alikuwa ameghafilika mno na Siku ya Kiyama na juu ya kuhudhurishwa kwenye hadhara hiyo nzito itakayoamua hatima yake ya milele; na atatambua pia kuwa hakuweza kujiandaa na majibu ya kwenda kutoa kwa masuali atakayoulizwa siku hiyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuyakimbia mauti ni sifa ya kimaumbile ya mwanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, sakaratul-mauti ni hali inayowapata watu wote. Hofu, mshtuko na mbinyo wa kifo vina uzito wa namna ambayo humfanya mtu apoteze uwezo na hali yake ya kawaida pamoja na umaizi na umakini wa mambo. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, kughafilika na akhera ni hatari inayomkabili mwanadamu na kumfanya atekwe na aikumbatie dunia na mapambo yake laisal kiasi, ikiwemo kushughulishwa zaidi moyo wake na mke au mume na watoto wake. Wa aidha aya hizi zinatutaka tutambue kuwa, dunia na mapambo yake ni mithili ya pazia na utando unaoziba uonaji wa mtu na kumkosesha kuiona haki. Kwa hiyo mtu aliyeghafilika, huwa hana uonaji wa kina. Lakini Siku ya Kiyama, wakati vizuizi hivyo vitakapoondoka, mwanadamu atarejea kwenye hali ya umaizi na umakini kamili na kubainikiwa na hakika mpya ya mambo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 950 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atufanyie wepesi katika sakaralatul-mauti zetu, atuondolee pazia la mghafala juu ya Kiyama na Akhera ndani ya nyoyo zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Walaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/