Kumbukumbu ya kufa shahidi Fatima Zahra (as)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki maalumu kinachokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatima Zahra (a.s) binti mtukufu wa Mtume Muhammad (s.a.w).
Awali ya yote tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote ulimwenguni hususan wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) kwa manasaba huu. Katika dakika hizi chache tutatupia jicho kwa mukhtari historia ya maisha ya mtukufu huyu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki maalumu.
Tarehe 3 Jamadi Thani mwaka wa 11 Hijria yaani ikiwa imepita miezi mitatu tu na ushei tangu kufariki dunia Bwana Mtume SAW, ilikuwa ni siku ambayo Bibi Fatma Zahra AS alizidiwa na maradhi na huzuni kubwa kutokana na masaibu na mabalaa aliyokumbana nayo tangu alipoaga dunia baba yake kipenzi na kurejea kwa Mola wake. Kwa hakika hizi zilikuwa lahadha na nyakati za mwisho za umri uliojaa baraka wa binti huyu wa Bwana Mtume ambaye ni mke wa Imam Ali AS na mama wa Imam Hassan na Hussein AS. Huzuni na ghamu ya kuondokewa na baba yake kipenzi kwa upande mmoja, na masaibu aliyokumbana nayo baada ya kifo cha baba yake mtukufu kwa upande wa pili, yalimlemaza kiafya na kumfanya ashindwe kuamka kutoka katika tandiko lake.
Hebu turejee Yuma kidogo katika masiku ya baada ya kufariki dunia baba yake. Bibi Fatima Zahra (a.s) alikuwa na majukumu na masuuliya makubwa. Kwa hakika Fatima Zahra alikuwa mwanamke aliyejipamba kwa sifa za kipekee ambazo zilimtofautisha na wanawake na wanaume wote isipokuwa Mtume saw na Imam Ali bin Abi Twalib as. Mwanamke mwema huyu alijipamba na sifa zote njema na kufikia daraja ya juu ya uchaji Mungu.

Mtume saw Amenukuuliwa akisema:"Kila mara Fatima alipokuwa akisimama katika mihrabu na mbele ya Mwenyezi Mungu, nuru yake ilikuwa ikiwaangazia Malaika mbinguni kama vile nuru ya nyota inavyowaangazia watu wa ardhini; na Mwenyezi Mungu husema: Enyi Malaika wangu mtazameni mja wangu Fatima, kiongozi wa waja wangu ambaye amesimama mbele yangu na mwili wake unatetemeka kwa khofu juu yangu na anafanya ibada kwa ajili yangu hali ya kuwa moyo wake umejaa khofu, unyenyekevu na khushui. Ninakushuhudisheni kwamba, nimewapa amani wafuasi wake kunako moto wa Jahanamu."
BibiFatima Zahra (as), ni binti wa Nabii Muhammad (saw) na Hadhrat Khadijah binti Khuwailid (sa), mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na mama wa Imam Hassan na Hussain (as). Bibi Fatima ana nafasi ya juu sana katika Uislamu na amepambwa kwa sifa nyingi. Baada ya mumewe, Ali bin Abi Twalib (as), maimamu wengine kumi na mmoja wa Ahlul Bait (as) wanatoka katika kizazi chake, na Sura na Aya kadhaa za Qur'ani kama vile Suratul Kauthar, Suratul Insan, Ayatu al Tat'hir, na Ayatul Mawaddah ziliteremshwa kuhusiana naye, mume wake na watoto wake.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, anasema kuhusu hali ya kiroho ya Bibi Fatima al Zahra (as) na jinsi alivyokuwa "Muhaddatha" kwamba: "Fatimatu Zahra (as) ni mtu ambaye alikuwa akizungumzishwa na maelfu ya Malaika wa karibu na Mwenyezi Mungu alipokuwa akisimama kwenye mihrabu ya ibada, wakimsalimu, kumpongeza na kumwambia maneno yaleyale yaliyokuwa yakisemwa na Malaika kwa Bibi Maryam mtakatifu.
Akitaja sifa na matukufu ya Zahraul Batul (as), Ayatullah Khamenei pia amesema: “Imepokewa katika Hadith kwamba, Hadhrat Maryam alikuwa kinara wa wanawake wa ulimwengu wa zama zake, lakini Fatima Zahra ni kinara na bibi wa wanawake wa ulimwengu katika vipindi vyote vya historia. Alifikia daraja za juu za kiroho kiasi kwamba Malaika walikuwa akizungumza naye katika kipindi cha ujana wake na kumfunza mambo mengi kwa kadiri kwamba alijulikana kuwa ni "Muhaddatha".
Bibi Fatimah (a.s.) ni mwanamke anayezingatiwa kuwa ni wa kutolea mfano katika dini ya Kiislamu, na pia ni kiigizo chema kwa kila mwanamke anayetafuta mafanikio katika maisha yake. Bibi Fatima binti Muhammad (s.a.w.w) ndiye mwanamke bora ulimwenguni aliyezaliwa na kupata malezi katika nyumba iliyokuwa ikishuka ndani yake Wahyi kutoka mbinguni. Si hivyo tu, bali Bibi Fatima alihitimu mafunzo ya Uislamu katika madrasa ya Utume, na kutokana na mafunzo hayo aliweza kufikia daraja ya juu na tukufu. Katika kuthibitisha ubora wa Bibi Fatima, Mtume (s.a.w.w) amepata kusema, "Hakika Mwenyezi Mungu huwa radhi kwa kuridhia Fatimah, na huchukia kutokana na kuchukia kwa Fatima.Kutokana na daraja kubwa aliyonayo Bibi Fatimah katika Umma wa Nabii Muhammad (s.a.w.w) imekuwa ni wajibu kwa kila mwanamke duniani kuiga mwenendo wa Bibi huyu katika maisha yake, ajing'arishe kwa nuru yake nzuri na afuate nyayo zake ambazo zitamuelekeza kwenye mafanikio na utukufu.

Pamoja na adhama na utukufu wote huo, lakini msiba mkubwa wa baba yake pamoja na masaibu, maudhi aliyoyapata na dhulma aliyofanyiwa baada ya baba yake kufariki dunia ni mambo yaliyomvunja na kumtesa mno bibi Fatima AS. Muda mfupi baada ya baba yake kuaga dunia, alikumbana na maudhi na dhulma ya baadhi ya wale wanaodai kuwa ni Waislamu ambayo yalimfanya apoteze ujauzito wake na kubakia kitandani akiwa mgonjwa asiyejiweza.
Bibi Fatimatu Zahra (a.s.) alisema wakati anamuaga mumewe, Amirul Muminin (as) kwamba: "Ewe Abul Hasan! Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliniahidi na kuniambia kwamba mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuungana naye, na hapana budi hili litatimia. Hivyo basi kuwa na subira mbele ya amri za Mwenyezi Mungu Mkubwa, na uridhie hukumu yake."
Imenukuliwa kwamba Imam Ali bin Abi Twalib na masahaba kadhaa waliokuwa karibu sana na familia ya Mtume waliuzika mwili wake usiku mkubwa kama alivyokuwa ameusia yeye mwenyewe, ili wale waliomdhulumu wasishiriki mazishi yake. Wakati anauweka mwili wake kaburini, Imam Ali (as) alisema maneno ya huzuni akimhutubu Mtume (saw). Sehemu moja ya maneno hayo inasema:
Sala na salamu za Allah ziwe juu yako Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kutoka kwangu na kwa binti yako anayekuja kwako na kuungana na wewe haraka... Amana uliyoniachia imerejeshwa, lakini huzuni yangu itabakia milele, na nyakati za usiku nitabakia macho hadi Mwenyezi Mungu atakaponichagulia nyumba yako unakoishi wewe kwa sasa. Binti yako atakupa habari kuhusu jinsi umma wako ulivyoungana kwa ajili ya kumdhulumu. Hivyo basi muulize yaliyojiri na yaliyotupata baada yako.....
Muda wa kipindi hiki maalumu umefikia tamati. Natumai mmenuufaikak na yale niliyokuandalieni kwa leo. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.