Jul 18, 2024 09:09 UTC
  • Podikasti ya Ujana Ulioharibiwa- Sehemu ya 8

Sehemu hii ya nane ya Podikasti ya Ujana Ulioharibiwa (Stolen Youth) inaangazia vitendo vya mabavu na ubaguzi wa jeshi la Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Podikasti hii inaeleza yale yaliyoandikwa na Catherine Cook katika kitabu cha "Stolen Youth". Cook amefafanua hali ya mahakama na magereza za Israel wanakofungwa watoto wa Kipalestina na ukiukaji wa kimfumo wa haki na mikataba ya kimataifa inayohusiana na watoto unaofanywa na Israel kama kuwakamata, kuwatesa na kuwafunga jela watoto wa Kipalestina. Anasema utawala ghasibu wa Israel hauwashambulii bila sababu watoto wa Kipalestina wasio na ulinzi, bali lengo lake ni kuwakandamiza na kuzima vuguvugu dogo kabisa la malalamiko na mapambano ya watoto hao ili wasijiunge na harakati za mapambano ya ukombozi katika siku zijazo.   *****                       

Kama tulivyoeleza katika sehemu kadhaa zilizotangulia za podikasti hii, kwa miaka mingi sasa jamii ya kimataifa iimefafanua viwango vya kimataifa vya namna ya kuamiliana na watoto kwa mujibu wa vigezo vilivyoanishwa, hasa watoto walionyimwa uhuru wao. Msingi wa vigezo hivyo uliasisiwa mwaka 1989 baada ya karibu nchi zote wanachama, ukiwemo utawala wa Israel, kupasisha tamko la kutetea haki za watoto (CRC). Usahihi wa kauli na ushahidi wa yanayowapata watoto wa Kipalestina wanaofungwa jela na Israel umethibitishwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Palestina, kimataifa na Israel na yanaashiria visa vingi vya ukiukwaji wa sheria za kimataifa. Watoto wa Kipalestina ambao wamewahi kufungwa katika jela na korokoro za Israel kwa miongo kadhaa, bado wana kumbukumbu zenye kufanana kuhusu waliyokumbana nao wakati wakusailiwa. Kwa mujibu wa kauli hizo, utawala wa Israel huwafanyia ukatili, kuwadhalilisha na kuwatisha watoto wa Kipalestina pale wanapowakamata, wakati wa kuwahoji, kuwahukumu na kuwafunga jela. Israel inakiuka wazi sheria za haki za binadamu kwa kutumia mifumo miwili tofauti ya mahakama kwa Wapalestina na watu wa Israel. Sheria ya kiraia ya Israel inayotumika kuhusu raia wa utawala huo haramu ni tofauti sana na maagizo ya kijeshi yanayotumika kwa Wapalestina. Mfumo huo wa kindumakuwili wa Israel unahalisha ubaguzi. 

Raia wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu wanatendewa tofauti kabisa na sheria kwa sababu ya utaifa wao. Ni dhahir shahir kuwa dhati ya Israel ni ya kibaguzi kikamilifu, na  mfumo huu rasmi wa serikali wa ubaguzi, kama inavyothibitishwa na ushahidi wa maelfu ya wafungwa wa Kipalestina, ikiwa ni pamoja na watoto, si tu kwamba ni mwenendo mbaya na wa aina yake, bali ni mkakati ambao ulijengeka kwa misingi ya ukandamizaji na utumiaji mabavu. 

Utawala wa Israel unaendeleza ukatili na ukandamizaji wake dhidi ya Palestina kwa kukiuka wazi  kanuni za Mkataba wa Haki za Mtoto. Israel inakiuka kanuni za msingi kuhusu haki za watoto wakati wa kuwatia mbaroni ikiwa ni pamoja na kuwanyima sehemu kubwa ya haki zao. Haki kama kuwatendea watoto hao kama raia wasio na hatia hadi tuhuma zinazowakabili zitakapothibitishwa, kujuzwa tuhuma zinazowakabili,  kutokamatwa kiholela na kinyume cha sheria, haki ya kupewa wakili wa utetezi, kuamiliana na watu wanaoandamana na mtuhumiwa kwa heshima, kutoa taarifa kwa familia yake na vilevile kuhusu mahali anaposhikiliwa. Watoto wanaotiwa nguvuni na Israel wananyimwa haki hizi za kimsingi.

Kwa kawaida wanajeshi wa Israel huwakamata watoto wa Kipalestina huku wakiwa wamewaziba nyuso zao jambo ambalo linakiuka sheria za kimataifa. Jambo lililo wazi hapa ni kuwa wale wanaotekeleza amri ya kuwaweka kizuizini watoto wanapasa kuwatendea kwa njia inayofaa kulingana na umri na pia mahitaji yao. Kwa maana kwamba, kuna ulazima wa kutumiwa njia na mbinu mahsusi kwa ajili ya watoto. Hata hivyo utawala wa Israel hauheshimu vigezo vyovyote vya kimataifa na unatekeleza vitendo vya kikatili na mateso kwa kundi hilo. 

Jeshi la Israel mwezi Julai 1967 lilitoa dikri ambayo iliwaondoa walowezi wa Kiyahudi katika maagizo ya kijeshi yaliyokuwa yakitolewa kwa ajili ya Wapalestina. Ni wazi kuwa walowezi wa Kiyahudi wanalindwa chini ya mwavuli wa sheria ya kiraia ya Israel. Hata walowezi haramu huwa na haki zaidi kuliko Wapalestina pale wanapofanya uhalifu. 

Kanuni ya Mkataba wa Haki za Mtoto inamtaja mtoto kuwa ni binadamu yeyote aliye na umri wa chini ya miaka 18. Israel pia ni mojawapo ya pande zilizosaini kanuni hiyo. Hata hivyo, kivitendo, utawala huo bandia unawahesabu watoto walio na umri wa miaka 16 na kuendelea kuwa watu wazima. Matokeo ya mtazamo huu yanaweza kushuhudiwa katika mahakama za watoto, hukumu zinazotolewa dhidi yao na pia pale wanapokamatwa na kufungwa katika jela zinazosimamiwa na jeshi la Israel. Jambo la kuhuzunisha zaidi kuhusu matendo ya Israel ni ubaguzi katika kutoa hukumu. Hapa tunaashiria mifano michache ya ubaguzi huo. 

Jeshi la Israel Septemba 15 mwaka 2000 lilimtia nguvuni Murad Rashid Abu Judeh. Israel ilimtuhumu Abu Judeh kuwa amewarushia mawe  wanajeshi wa utawala huo. Mahakama ya kijeshi ilimhukumu Mpalestina huyo kifungo cha miezi 10 jela katika gereza la kijeshi la Megiddo na faini ya NIS 3,000 yaani dola za Marekani takriban (690). Mkabala wake,  tarehe 30 Septemba mwaka 1988 Rabi wa Kiyahudi aitwaye Moshe Levinger aliwafyatulia risasi watu kadhaa katikati mwa mji wa Hebron. Kuhani huyo wa Kiyahudi alimuuwa Mpalestina mmoja na kumjeruhi mwingine. Aprili 12 mwaka 1989 mahakama ya Israel ilimpata na hatia ya kosa la kuuwa, kusababisha madhara makubwa ya mwili katika mazingira magumu, na kusababisha uharibifu kwa nia mbaya. Hata hivyo mwezi Mei 1990 kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya mwendesha mashtaka wa eneo la Baitul Muqaddas na wakili wa Lavinger, alihukumiwa kutumikia kifungo cha miezi mitatu tu jela! 

Katika kisa kingine cha ukandamizaji, wanajeshi wa Israel Novemba 15 mwaka 2000 walimtia nguvuni Mpalestina Sami Issa Qandil aliyekuwa na umri wa miaka 14. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulimtuhumu Qandil kuwa amewarushia mawe askari wa utawala huo. Wanajeshi wa utawala huo walimfunga mikono  na kumziba macho na kumpeleka katika kitongoji cha walowezi wa Kiyahudi. Polisi wa Israel walimsaili mtoto huyo wa Kipalestina katika kitongoji hicho. Walimpiga na kumwambia kwamba hawataacha kumpiga hadi akiri makosa. Baada ya Sami kulazimika kukiri tuhuma alizobambikiwa na polisi wa Israel walimpeleka katika korokoro ya Bait El katika Ukingo wa Magharibi na kumshikilia kwa siku tatu. Kisha wanajeshi wa Israel walimhamishia Sami katika korokoro ya Itzion karibu na Bait Laham na kusalia huko kwa muda wa wiki mbili. Baadaye mtoto huyo wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 14 alipelekwa huko Telmond  na kuwekwa pamoja na wafungwa wahalifu vijana wa Israel. Malalamiko ya wakili wa Sami kwa uongozi wa gereza pia hayakuwa na matokeo isipokuwa kupigwa zaidi na wafungwa wa Israel. Hatimaye mahakama ya kijeshi ya utawala bandia wa Israel ilimhukumu Sami kifungo cha miezi 6 jela na miezi 10 ya kifungo kilichosimamishwa.. Sami alikaa miezi miwili katika jela ya wahalifu wa Israel na hakuthubutu hata kulala akihofiwa kushambuliwa na wafungwa wengine. 

Katika upande mwingine, Margalit Har-Shefi, alihukumiwa mwaka 1998 kwa kosa la kujua njama ya mchumba wake wa zamani, Yigal Amir ya kumuua Waziri Mkuu wa wakati huo wa Israel, Yitzhak Rabin mwaka 1995 na kutotoa taarifa kwa polisi. Har-Shefi alihukumiwa kifungo cha miezi 9 jela, hukumu aliyoanza kuitumikia mwezi Machi 2001. Mwezi Julai mwaka huo huo, Rais wa Israel Moshe Katsav alimpunguzia kifungo hadi miezi 6. Akitetea hatua hiyo, Katsav alisema kuwa Margalit Har-Shefi ametimiza wajibu wake kwa jamii, ameadhibiwa na kwamba amehuzunishwa na mauaji ya Waziri Mkuu na kuyalaani. 

Mifano hii michache inatosha kuonyesha kiwango cha mienendo ya ubaguzi inayoshuhudiwa kati ya Mpalestina na Muisraeli. *****

Sheria za Kiraia za Israeli pia zinatofautisha kati ya watoto wa Israel na watu wazima katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) katika mfumo wa mahakama. Ni wazi kuwa sheria maalumu zinapaswa kuzingatiwa katika kushughulikia kesi za watoto wahalifu na mabarobaro wa Israel. Mamlaka husika zinazoshughulikia watoto wa Israeli zinatakiwa kufuata maagizo ya ndani kuhusu taratibu za kisheria za watoto. Israel ilisema katika ripoti yake kwa Kamati ya Haki za Watoto ya Umoja wa Mataifa mwaka 2001 kwamba: "Masuala ya watoto na mabarobaro katika aghalabu ya kesi yanashughulikiwa na watu ambao wamepata mafunzo maalumu. Katika mifumo yote kuna sheria ambazo lengo lake ni kuwahami watoto na mabarobaro... Kila mtoto huwa anaongozana na wataalamu wa matibabu kuanzia mwanzo wa mchakato wa mahakama. Maamuzi mengi yanayohusiana na mustakbali wa watoto hao huchukuliwa kupitia mashauriano lengo kuu likiwa ni kuwarekebisha na kuwarudisha katika jamii..." 

Hii ni katika hali ambayo Israel kamwe haifanyi hivi kwa watoto na mabarobaro wa Kipalestina. Kwa maneno mengine ni kuwa, ni watoto wa Israel pekee, na si watoto wa Kipalestina, wanaohukumiwa katika mahakama maalumu za watoto au zile ambazo zinasimamiwa na majaji maalumu wa watoto. Ni dhahir kuwa, mahakama za kijeshi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hazina mfumo kama huo. Watoto wa Kipalestina wanafikishwa katika mahakama zilezile ambazo hushughulikai kesi za watu wazima. Jeshi la Israel linabagua hata katika kuwakamata watoto wa Kipalestina na wale wa Israel. 

Mbali na hili, hatua ya Israel ya kuwakamata na kuwatia nguvuni watoto wa Palestina inasababisha pia mashinikizo kwa jamii nzima ya Wapalestina. Israel imekuwa ikizidisha kamatakamata na kuwatia nguvuni raia wa Palestina pale inapokabiliwa na hali mbaya ya kisiasa. Sababu ya kukamatwa si lazima iwe ya kisasa, bali kitendo cha kuwa Mpalestina hasa kwa wanaume na watoto wa kiume ni hatari kwa upande wa Israel. Ukweli kwamba, kila raia wa kiume wa Palestina anaweza kutiwa nguvuni wakati na mahali popote unaisababishia jamii mashinikizo makubwa ya kiakili na kinafsi. Hata hivyo mashinikizo hayaishi hapo, bali taarifa za watu kuhusu hali ya jela za utawala wa Israel zinazidisha mashinikizo hayo. Hii ni kwa sababu, Wapalestina wanajua kuwa haiwezekani mfungwa kupewa ruhusa ya kukutana na kuzungumza na familia yake. Aidha mfungwa hunyimwa msaada wa utetezi wa kisheria na wale wanaoshikiliwa jela huwa katika hali ngumu sana. Israel inatuma ujumbe mkali kwa jamii ya Wapalestina kupitia njia hizi za kuwatia nguvu raia hao kwamba, muqawama na mapambano dhidi ya Israel vina gharama kubwa. 

Ukatili wa Israel kwa wafungwa watoto wa Kipalestina unatokana na kuongezeka uhasama na si kitendo cha sadfa. Swali linalojitokeza ni kwamba je, Israel inafuatilia lengo gani kwa kufanya ukatili huu dhidi ya watoto wa Kipalestina?

Utawala wa Israel unamchanganya na kumtia hofu mtoto aliyewekwa kizuizini wa Kipalestina kwa kutumia mbinu za mateso ya kimwili na kisaikolojia. Kwa nini? Jibu liko wazi kabisa; kumlazimisha mfungwa huyo wa Kipalestina kukiri makosa aliyobambikiwa katika muda mfupi kadiri iwezekanavyo.

Utaratibu huu unafanywa kwa kukariri tuhuma zinazomtambua mtoto huyo kuwa nui mhalifu. Mbinu mseto za mateso kwa kawaida humlazimisha mfungwa kutia sahihi maungamo ambayo huwa msingi wa kutiwa hatiani katika mahakama za kijeshi za Israel. Ni vyema kukumbusha hapa pia kwamba, taratibu nzima za amri za mahakama za kijeshi zimebuniwa kwa shabaha ya kudumisha utawala wa Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hivyo huo bora kuanza kazi hii na watoto wa Kipalestina ili woga uingie ndani ya nyoyo zao tangu utotoni na wasifikirie kupambana nao hata kidogo. Kwani, kwa Israeli, kila Mpalestina anatambuwa kuwa tishio la usalama.

Haya yote yanajiri katika hali ambayo, hakuna taasisi ya ndani au kimataifa inayoweza kuuchukulia hatua utawala wa Israel. Utawala wa Israel haujawahi kuwa na nia ya kubadili siasa zake na kuamiliana kibinadamu na wafungwa wa Kipalestina. Badala yake, Israel imeendelea kuwa mwanaminifu kwa hila na mbinu zake za siku zote kwa kudumisha rasmi mfumo wake wa ubaguzi, ukandamizaji na ukatili dhidi ya Wapalestina. 

Tags