Nov 09, 2016 11:27 UTC
  • Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa

Tarehe 13 mwezi Aaban mwaka wa Hijria Shamsia ambayo mwaka huu inasadifiana na tarehe 3 Novemba, inatambuliwa hapa nchini Iran kama Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa.

Siku hiyo ilishuhudia matukio kadhaa kwa miaka mitatu tofautui ambayo kwa njia moja au nyingine yalihusisha Marekani, beberu mkubwa zaidi duniani katika zama hizi. Siku hiyo ya tarehe 13 Aaban mwaka 1343 Hijria Shamsia yaani mwaka 1964, askari wa utawala wa Shah walimtia nguvuni Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kumpeleka uhamishoni nchini Uturuki, kwa sababu Imam alikuwa akipinga vikali utawala kibaraka wa Shah na uingiliaji na ushawishi mkubwa wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran. Miaka 14 baadaye yaani mwaka 1978 wakati harakati za Mapinduzi ya Kiislamu zilipokuwa zikipamba moto zaidi siku baada ya siku na katika siku kama hiyo hiyo ya tarehe 13 Aaban, kundi la wanafunzi lilifanya maandamano kupinga hatua ya utawala kibaraka wa Shah ya kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini na sera za ukandamizaji za utawala huo. Maandamano hayo yalishambuliwa na kukandamizwa kinyama na utawala wa Shah na wanafunzi wengi wakauawa shahidi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini katika kumbukumbu ya tukio hilo chungu na wakati wanafunzi walipokuwa wakiandamana kupinga siasa za kibeberu za Marekani na uingiliaji wa nchi hiyo katika masuala ya ndani ya Iran, ubalozi wa Marekani mjini Tehran ambao ulijulikana kwa jina la Pango la Ujasusi dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu, ulivamiwa na kutekwa na wanafunzi wa vyuo vikuu. Tukio hilo lilitajwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini kuwa lilikuwa "Mapinduzi ya Pili", baada ya Mapinduzi ya Kiislamu yaliyouangusha utawala dhalimu wa Shah nchini Iran.  

Kwa mnasaba wa Siku hiyo ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa, kila mwaka taifa la Iran hufanya sherehe mbalimbali za kuadhimisha siku hiyo ili kudumisha sifa ya kupambana na ubeberu. Hata hivyo kabla ya kwenda mbali zaidi tunapaswa kujiuliza kwamba, istikbari au ubeberu ni nini? Na kwa nini hii leo tunaitambua Marekani kuwa ndiyo dhihirisho la ubeberu?

Neno "istikbar" linalotumiwa kueleza ubeberu, linatokana na asli ya "kibr" katika lugha ya Kiarabu ambalo lina maana ya kiburi, ghururi na tabia au ugonjwa wa kupenda makuu (Megalomania). Katika kufafanua zaidi wa istilahi hiyo ya Qur'ani, wataalamu wanasema kuwa: Istikbari ni mtu kujifanya mkuu na kuyatambua yote yasiyo yake au asiyostahiki kuwa ni yake yeye. Neno Istikbar limetumiwa mara 48 katika aya za Qur'ani tukufu kwa ajili ya vitu na watu mbalimbali kama Shetani, Firauni, Qarun na Haman. Hata hivyo wa kwanza kabisa kujifanya mkuu alikuwa Iblisi mal'uni. Aya ya 34 ya Suratul Baqarah inasema: Na kumbuka tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri. 

Uistikbari wa Iblisi na mustakbirina na mabeberu wengine unatokana na kujiona wakuu na bora zaidi ambako hatimaye kuliwaporomosha na kuwafanya wamuasi Mola wao Muumba. Sifa hiyo mbaya inaonekana katika mifano yote iliyotolewa na Qur'ani tukufu kuashiria watu wa aina hiyo na katika mabeberu na mustakbirina wote waliotokea katika historia ya mwanadamu. 

Wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na baada yake pia Imam Ruhullah Khomeini alitumia istilahi hiyo ya Qur'ani kuonesha sura na hulka ya maadui halisi wa wananchi na Mapinduzi na kuzitaja Marekani na Urusi ya zamani kuwa ndio vielelezo vya mustakbirina na mabeberu wa zama hizo. Pamoja na hayo Imam Khomeini alikuwa akisisitiza kuwa, Marekani ndiye shetani mkubwa na hatari zaidi. Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani hapo mwaka 1991, Marekani ilidhihirika zaidi kama dola la kibeberu na linalopenda makuu zaidi na zaidi. Ni kweli kwamba baadhi ya madola ya Ulaya pia yana tabia na maradhi haya ya kujiona makuu na hulka za ubeberu, lakini taathira ya nchi hizo si kubwa kama ile ya Marekani. 

Mapambano dhidi ya mabeberu yanaendelea

Kutokana na tabia hiyo ya kupenda ukuu na kujitambua kuwa juu na bora zaidi, madola ya kiistikbari na kibeberu hususan Marekani yanajipa haki ya kuzifanyia nchi nyingine jambo lolote lile linalopingwa na kupigwa vita na ubinadamu na sheria za kimataifa. Hulka ya unyonyaji na kutaka kujilimbikiza kila kitu ambayo ina mizizi katika fikra za kiliberali za Magharibi imezifanya nchi hizo za kibeberu zilipe kipaumbele zaidi suala la kupora utajiri na maliasili za nchi nyingine.

Tabia ya kupenda kuzidhibiti na kuzitawala nchi nyingine ni matokeo mengine ya ubeberu ambayo huandamana na kujiona bora na juu ya wengine na hutumika kwa ajili ya kudhamini maslahi haramu ya dola la kibeberu. Katika miaka ya huko nyuma tabia hii ya kudhibiti na kuzitawala nchi nyingine ya nchi za Magharibi ilishibishwa kwa kizivamia na kuzikoloni nchi na mataifa mengine, kupora utajiri na malisi zao na kufanya ukatili wa kutisha, lakini katika zama hizi Marekani na wenzake wanaendeleza tabia na hulka hiyo kwa sura mpya. Matokeo ya hulka na sera hiyo ya kibeberu ni kuyabakisha nyuma kimaendeleo mataifa yanayodhibitiwa na kuzuia maendeleo, ustawi na kujitawala kikamilifu kwa nchi na mataifa hayo. Pamoja na hayo, mabeberu na mustakbirina wanajua vyema kwamba, kutokana na ukatili na sera hizo za kinyama yumkini wakakabiliwa na hasira na mapambano ya watu na mataifa mbalimbali; kwa sababu hiyo huogopa na kupatwa na wahka kutokana na harakati za watu wanaodhibitiwa na madola hayo. Ili kuzuia harakati na mapambano ya watu, madola hayo ya kibeberu hutumia njia kama zile za kuzusha hitilafu na migawanyiko baina ya watu, makundi au makabila ya nchi na eneo husika, kueneza ufuska na ufisadi, kuitenga nguvu kazi hodari na inayowajibika na kutumia vibaraka wa ndani na wanafikra au wasomi waliotekwa na fikra za kimagharibi.

Kwa kutilia maanani sifa na tabia hizo za istikbari na ubeberu, inaonekana wazi kuwa, kupambana na kusima kidete dhidi ya ubeberu ni jambo linaloungwa mkono na kutiwa nguvu na akili, busara na mantiki. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, hakuna mwanadamu huru na mwenye akili timamu anayekubali kuishi katika dhulma na udhibiti wa upande mwingine sawa uwe ni mtu, dola au nguvu yoyote ya kimataifa. Vilevile dini inayopinga dhulma na uonevu ya Uislamu inawaamuru wafuasi wake wasikubali kuonewa na kudhulumiwa na vilevile inawataka kuwasaidia watu wanaodhulumiwa. Katika aya za kitabu kitukufu cha Qur'ani, Mwenyezi Mungu SW pia anawalaumu Waislamu waliozembea katika kuwasaidia wanaodhulumiwa na kukandamizwa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inajitambua kuwa inawajibika kutekeleza sheria za Uislamu, ikalizingatia vyema suala hilo katika kifungu cha 154 cha katiba yake kinachosisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kujiepusha kikamilifu na aina zote za kuingilia mambo ya ndani ya mataifa mengine, inaunga mkono mapambano ya kupigania haki ya watu wanaokandamizwa dhidi ya mabeberu katika kila kona ya dunia", mwisho wa kunukuu. Himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mataifa yanayodhulumiwa na kukandamizwa kama Palestina, Yemen, Syria, Iraq na kadhalika inatokana na asli na msingi huu.

Ni miaka karibu arubaini sasa ambapo taifa la Waislamu wa Iran linapambana na ubeberu wa Marekani na vibaraka wake katika eneo la Mashariki ya Kati na tajiriba na uzoefu huo mkubwa umeifanya Iran kuwa ngome na kituo kikuu cha mapambano dhidi ya madola ya kiistiimari. Mapambano na kusimama kidete kwa Jamhuri ya Kiislamu kuliilazimisha Marekani iombe mara kadhaa kufanya mazungumzo na Iran; hata hivyo kutokana na kuelewa tabia na hulka ya kibeberu ya Marekani, Iran imekuwa ikikataa ombi hilo. Pamoja na hayo katika miaka ya hivi karibuni viongozi wa Iran walikubali ombi la kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 linalojumuisha nchi kadhaa ikiwemo Marekani, licha ya kutoimani kabisa serikali ya Washington.

Hatua hiyo kwa hakika ilikuwa mtihani mkubwa kwa Wamarekani ili kuonesha ni kwa kiwango gani wanashikamana na kuheshimu makubaliano na kauli zao. Hususan kwa kutilia maani kwamba, Marekani na madola mengine ya Magharibi daima yamekuwa yakijitangaza kuwa yanaheshimu makubaliano ya pande mbili na sheria za kimataifa na kuzituhumu nchi nyingine kuwa ni wakiukaji wa sheria hizo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuhusu mazungumzo hayo kwamba: Kama tulivyokariri mara kwa mara, hatufanyi mazungumzo na Marekani kuhusu masuala mbalimbali ya kieneo na kimataifa. Hatufanyi mazungumzo kuhusu masuala ya pande mbili, lakini baadhi ya wakati na kwa nadra sana kama vile katika suala la nyuklia, tumefanya mazungumzo nao kwa mijubu wa maslahi...", mwisho wa kunukuu. Matokeo ya mazungumzo hayo ni makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo kwa mujibu wake, Iran ilikubali kusitisha baadhi ya miradi yake katika sekta ya kuzalisha nishati ya nyuklia mkabala wa Wamagharibi husuan Marekani kufuta vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Iran imetekeleza kikamilifu wajibu wake kwa mujibu wa makubaliano hayo na hilo limethibitishwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo Marekani na kutokana na hulka yake ya kibeberu na kutaka kudhibiti pande nyingine, imekataa kufuta kivitendo vikwazo dhidi ya Iran. Kwa utaratibu huo taifa la Iran limepata tajiriba na uzoefu mpya katika kupambana na ubeberu nao ni kuwa Marekani si tu kwamba haiheshimu maneno na kauli zake, bali pia haishikamani na kuheshimu sheria rasmi za kimataifa. Hali hii kama anavyosisitiza Ayatullah Khamenei, ndiyo hulka ile ya ubeberu ya kutaka kutumia mabavu, kujiona juu na bora na kupenda ukuu, ghururi na kiburi ambazo ndizo sifa za shetani na Iblisi. Kwa msingi huo Ayatullah Khamenei anasema: Mapambano dhidi ya ubeberu hayawezi kusitishwa na kusimamishwa... Hii ni miongoni mwa wajibu zetu kubwa, na miongoni mwa misingi na nguzo za Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa maana kwamba, kama hakutakuwepo mapambano dhidi ya ubeberu, basi tutakuwa hatuifuati  Qur'ani, na Marekani ndio kielelezo kamili cha ubeberu...", mwisho wa kunukuu.   

 

Tags