Wiki ya Umoja wa Kiislamu na Ujumbe wa Mtume (saw)
(last modified Tue, 05 Dec 2017 11:57:53 GMT )
Dec 05, 2017 11:57 UTC
  • Wiki ya Umoja wa Kiislamu na Ujumbe wa Mtume (saw)

Tumo katika kipindi cha Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Wiki hii ilitangazwa na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Ruhullah Khomeini kwa ajili ya kuimarisha umoja kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni ambao wanasherehekea Maulidi na kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (saw) katika siku mbili tofauti za tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki.

Katika kipindi hiki wapenzi wasikilizaji, tumo katika siku za kuadhimisha na kukumbuka tukio kubwa zaidi katika historia ya mwanadamu yaani siku ya kuzaliwa mbora wa viumbe Muhammad bin Abdullah SAW, Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu aliyekuja kukamilisha waliyokuja nayo Mitume wote wa kabla yake kama Ibrahim, Nuh, Mussa na Issa SA. Siku nyota ya Muhammad ilipochomoza katika anga ya Makka hakuna mtu wa kipindi hicho cha ujahilia kilichokuwa kimegubikwa na ujinga, dhulma, na upotovu aliyedhani kwamba, mtukufu huyo alikuwa na ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wanadamu wote. Muhammad aliyesifika kwa uaminifu, usafi na utakasifu alishika usukani wa kuongoza jahazi la binadamu wote kuwaelekeza kwenye bara la amani, hakika na haki yote. Nara yake kuu ilikuwa kuwaunganisha wanadamu, kufuta ujinga, kupambana na dhulma na uonevu na kujenga udugu baina ya waumini. Alijenga udugu baina ya Muhajirina kutoka Makka na Ansari wa Madina na akafutilia mbali kutu ya vinyongo na uhasama uliokuwepo kwa miaka mingi baina ya makabila ya Waarabu. Katika kipindi kifupi cha baada ya kutangaza ujumbe wake, Muhammad (saw) alitekeleza kikamilifu ujumbe wa aya ya 103 ya Suratu Aal Imran inayosema: Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyokuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu.  

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: Nabii Muhammad (saw) ni nguzo kubwa zaidi ya umoja wa Waislamu katika vipindi vyote vya historia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, itikadi ya Waislamu wote kwa mtukufu huyo inaandamana na upendo na mahaba ya aina yake, suala linalomfanya mtukufu huyo kuwa kibla na kituo kikuu cha nyoyo za wafuasi wake na kuzidisha mshikamano na ukuruba baina ya makundi yote ya Kiislamu", mwisho wa kunukuu.

Umoja na kuunga udugu ni miongoni mwa mbinu zilizotumiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw) kwa ajili ya kurekebisha misingi ya kifikra na kiitikadi ya Waislamu wa awali. Imepokewa kwamba, wakati mtume (saw) alipokuwa katika eneo la Nukhaila pamoja na masahaba zake wapatao 740, Malaika Jibril aliteremka kwa mtukufu huyo na kumwambia: "Mwenyezi Mungu SW amefunga mkataba wa udugu baina ya malaika wake." Kwa msingi huo Mtume (saw) pia aliamua kufunga mkataba wa udugu baina ya masahaba zake. Mtukufu huyo alifunga mkataba wa udugu baina ya Abu Bakr na Umar, baina ya Uthman na Abdur Rahman, baina ya Salman Farsi na Abu Dharr, baina ya Twalha na Zubair, baina ya Ammar bin Yasir na Miqdad, baina ya Mus'ab na Abu Ayyub al Ansari, baina ya Aisha na Hafsa, baina ya Ummu Salama na Safiya na kadhalika. Kisha Mtume Muhammad (saw) mwenyewe alifunga mkataba wa udugu baina yake na Ali bin Abi Twalib (as). (Biharul Anwar juzuu ya 38) Mkataba huo wa udugu ulikuwa imara na madhubuti kiasi kwamba, Mtume (saw) alitoa amri kwamba masahaba wawili waliokuwa wameuliwa shahidi katika vita vya Uhud kwa majina ya Abdullah bin Umar na Amru bin Jamuuh ambao walikuwa wamefunga mkataba wa udugu baina yao, wazikwe katika kaburi moja. (Nahjul Balagha-Sherhe ya Ibn Abil Hadid)

Jambo linalopaswa kutiliwa maanani hapa ni kwamba, Mtume Muhammad (saw) alikuja na ujumbe wa dunia nzima. Alikuja kufuta ujinga na dhulma na kuwashika mkono waanadamu na kuwaelekeza kwenye mwanga na ukamilifu. Hata hivyo dunia ya sasa iliyogubikwa na umaada inaonekana kulemewa na mizigo ya dhulma na ujinga mamboleo. Hivyo mwanadamu wa leo anahitajia zaidi hadiya ya masuala ya kiroho, Tauhidi na maarifa aali aliyotuletea mtukufu huyo kuliko kipindi kingine chochote hususan katika siku hizi za kuadhimisha na kusherehekea maulidi na kuzaliwa kwake. Muhammad Mwaminifu aliwalingania wanadamu udugu, upendo, amani kusaidiana na kushirikiana. Aliwataka kuwa huru kwa maana halisi ya neno hilo na kutokuwa mtumwa wa matamanio ya nafsi zao au kwa mtu mwingine yeyote. Aliwalingania itikadi ya Tauhidi na kutokuwa mjaa na mtumwa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu Mmoja. Aliwaamuru kulinda uadilifu, kupambana na dhulma na uonevu na kuwasaidia wanadamu wanaodhulumiwa na kukandamizwa. Mafundisho haya na Nabii Muhammad (saw) yanahitajika sana katika dunia ya sasa inayozongwa na sera za watawala madhalimu, sera za kijuba za madola ya kibeberu na vibaraka wao wanaojiita Waislamu katika nchi za Waislamu. Haya ndiyo mambo ambayo iwapo Waislamu watashikamana nayo barabara wataweza kujikomboa kutoka kwenye minyororo ya ujahilia mamboleo na kumkomboa mwanadamu na dunia ya leo.

Mtume wa Mwisho, Muhammad (saw) aliondoa ukabila na fikra za kikaumu zilizokuwa zikiwagawa wanadamu na kusababisha uhasama na vita vya mara kwa mara na kujenga uhusiano mpya baina ya waumini uliotegemea imani ya Mungu Mmoja na matukufu ya kibinadamu. Imani na itikadi hiyo ilipewa jina la Uislamu na wafuasi wake wakaitwa Waislamu. Misingi mikuu ya dini hiyo aliyokuja nayo Mtume huyo wa mwisho wa Mwenyezi Mungu ilikuwa Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mmoja, kuamini siku ya mwisho na malipo na kumwamini mtukufu huyo kama Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu. Kila mtu aliyekubali na kuamini mambo hayo matatu aliitwa Mwislamu na kulazimika kulinda na kuchunga sheria na kanuni kadhaa.

Katika kanuni za Mtukufu Mtume (saw), Mwislamu wa kweli ni yule ambaye wanadamu wenzake wanasalimika na ulimi na mikono yake, kwa maana ya mtu asiyedhulumu wala kuwaudhi wanadamu wenzake. Dhulma, wasikilizaji wapenzi, katika sura zake zote ni dhambi kubwa isiyosameheka kirahisi. Kupora na kukanyaga haki za wanadamu wenzako, kuchupa mipaka yao kwa kuvuruga amani, kudhuru afya zao, kuwasababishia matatizo ya aina mbalimbali ya kimwili na kinafsi, na zaidi ya yote kuzusha mifarakano na hitilafu na uhasama baina yao ni kinyume kabisa na maadili na mafundisho ya Uislamu. Mtume Muhammad (saw) anasema katika moja ya hadithi zake kwamba: Mwislamu ni ndugu wa Mwislamu mwenzake, hamdulumu wala hamuudhi kwa matusi. Ni wazi kuwa, jambo lenye umuhimu mkubwa zaidi ya kuunga udugu ni kulinda udugu huo wenyewe. Hadithi zilizopokewa kutoka kwa mtukufu huyo zinawahimiza sana Waislamu kujali na kuimarisha udugu baina ya Waislamu na kuwakemea wale wanaokata mfungamano huo mtukufu.

Masjidu Nabi, Madina

Usaliti, kusema uongo, kutomsaidia mwanadamu mwenzako na mfano wake vinazuia umoja, upendo, mshikamano na ukamilifu wa jamii ya Kiislamu. Mtume (saw) anasema: "Mwislamu ni ndugu ya Mwislamu mwenzake, hapaswi kumsaliti, kumwambia uongo na kuacha kumsaidia."

Katika utamaduni wa mafundisho ya Mtume (saw) Mwislamu anapaswa kuwa kioo cha ndugu yake mwislamu. Kwa maana kwamba, anapasa kuona na kuakisi mazuri na mema yake na kumuonesha na kumtahadharisha na yaliyo mabaya.

Vilevile Waislamu wanapaswa kusaidiana katika kuimarisha uchumi wa kila mmoja wao na jamii nzima ya Kiislamu na kutayarisha mazingira mazuri ya ustawi na maendeleo. Hii ni miongoni mwa masuala muhimu yanayohitajiwa sana na Umma wa Kiislamu katika zama hizi. Sisi sote tumesikia hadithi ya Mtume inayosema: Mtu anayeamka asubuhi bila ya kujali masuala ya Waislamu wenzake basi huyo si Mwislamu." Wasomi wanasema neno "masuala ya Waislamu" lina maana pana sana inayojumuisha masuala ya uchumi, siasa, elimu, jamii na kadhalika, hivyo Mwislamu hapaswi kughafilika na kuwasahau Waislamu wenzake katika kila hali.

Aya ya 29 ya Suratul Fath inaweka wazi sura na picha ya Mtume na Waislamu waliokuwa pamoja naye pale inaposema: Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. 

Wapenzi wasikilizaji Aya hii na makumi mengine ya aya za Qur'ani tukufu zote zinatoa ujumbe kwamba, umoja, mshikamano, kusaidiana na kupendana ndiyo siri ya mafanikio ya Umma wa Kiislamu mkabala wa maadui wanafanya kila liwezekanalo kuzima nuru ya Allah SW. Wassalam alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.   

Tags