Kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Sajjad AS
(last modified Sat, 21 Apr 2018 11:09:53 GMT )
Apr 21, 2018 11:09 UTC
  • Kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Sajjad AS

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika dakika hizi chache za kipindi hiki maalumu ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS mmoja kati ya Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad SAW. Ni matarajio yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi karibuni.

Tarehe 5 Shaaban ya kila mwaka inasadifiana na siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Hussein AS, Imam ambaye kwa upande mmoja alikuwa ni 'pambo la wafanya ibada' na kwa minajili hiyo akapewa lakabu ya 'Zaynul Abidiin', na kwa upande mwingine alifanya juhudi kubwa za kufikia malengo matukufu ya babu yake, Mtume Mtukufu Muhammad SAW ya kuwepo  utawala wa Allah SW katika pembe zote za dunia. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Tehran inachukua fursa hii kutoa mkono wa heri na baraka kwa Waislamu wote duniani, kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa mmoja kati ya Wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW.

Imam Ali bin Hussein AS alizaliwa tarehe 5 Shaaban mwaka 38 Hijria katika mji wa Madina na baba yake ni Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS na mama yake ni Bi. Shaharbanu, aliyekuwa mmoja wa mabanati wa mfalme wa Kiirani. Hali ya kisiasa katika zama za Imam Sajjad AS ilikuwa nyeti na tata mno, baada ya Imam Hussein AS kusimama kidete dhidi ya utawala fasiki wa Bani Umayyah na hatimaye kuuawa shahidi huko Karbala. Imam Hussein AS alipambana dhidi ya fikra za watu waliokuwa wanataka kuupotosha Uislamu, wakati ambao jamii ya Kiislamu ilikuwa imezama kwenye hofu na woga. Kwani kitendo cha kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW na kushikwa mateka watu wa familia yake, kilikuwa ni cha jinai isiyo na mfano. Kipindi cha Imam Sajjad AS kilisadifiana na kipindi cha harakati za kijamii.  Kipindi hicho kilikuwa kimegubikwa na kukithiri vitendo vya upotoshaji  wa sheria  za Kiislamu, kwani  utawala wa Bani Umayyah ulikuwa ukiwapotosha Waislamu kwa kuwapelekea  wapokezi waongo wa riwaya na wapotoshaji. Harakati za Imam Sajjad AS zilileta mabadiliko makubwa, kwani baadhi ya watu walifikiri kwamba, Imam AS alikuwa amejikita zaidi kwenye masuala ya kiibada tu, na kujiepusha na masuala ya kijamii na kidunia. Hali ngumu na mbinyo uliokuwa ukitolewa na Bani Umayyah kwa upande mmoja na hali ya kiutamaduni na kijamii iliyokuwa ikitawala kipindi hicho kwa watu waliokuwa mbali na mafunzo sahihi ya Kiislamu kwa upande wa pili, ilimuongezea  Imam Sajjad AS moyo na ari kubwa ya kuwalingania watu kwenye njia ya haki. Imam Ali bin Hussein AS aliamua kutumia mbinu mpya ya kimantiki na kibusara kwa lengo la kuhuisha fikra halisi ya Kiislamu.  Imam Sajjad AS aliamua kutumia mawaidha na dua kwa lengo la kufikia kwenye malengo ya kimaanawi na ya kiharakati. Alichukua hatua hiyo ili aweze kukabiliana na harakati za kimaada za watu wa zama hizo. Kwa hakika Imam Ali bin Zainul Abidiin AS alichukua njia sahihi na bora zaidi ya kutumia dua na nasaha ili aweze kufikisha itikadi, ujumbe na fikra sahihi, zilizokuwa zikihitajika kwa watu walioishi katika kipindi hicho.

Amani iwe juu yako Ewe Zaynul Abidin, pamoja la wafanya ibada

 

Moja ya nasaha zilizotolewa na Imam Sajjad AS wakati alipokuwa akitoa mawaidha kwenye Msikiti wa Mtume SAW katika siku za Ijumaa alisema: 'Jambo la kwanza atakalokutana nalo mja wa Allah akiwa kwenye barzakh, ni kuulizwa maswali kutoka kwa Malaika wawili waliotumwa na Allah SW kuhusiana na Mungu  aliyekuwa akimuabudu, Mtume aliyeteremshiwa, dini aliyokuwa akiifuata, kitabu alichokuwa akikisoma na Imam  aliyekuwa akimfuata.' Imam Sajjad AS alikuwa akibainisha kwa uwazi mkubwa itikadi ya asili ya Uislamu, yaani tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Utume, Kiyama na suala muhimu la Uimamu. Maimamu AS wanauelezea uimamu kuwa ndio huohuo utawala. Imam anayeelezwa hapa ni mrithi wa Mtume Mtukufu SAW, yaani shakhsia adhimu  anayebeba jukumu la kuwaongoza watu katika masuala ya kidini na ya kidunia, na bila shaka kumtii yeye ni wajibu kwa Waislamu wote, kama ilivyokuwa sawa na kumtii Mtume Mtukufu SAW. Watu katika zama hizo walikuwa mbali na mafundisho ya Uislamu na kufikiri kwamba mtu mmoja anatawala katika masuala ya kidunia na mwingine anatawala katika masuala ya kidini. Bila shaka  mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Imam Sajjad AS yalikuwa yakiwakera na kuwachukiza mno makhalifa na viongozi wa Bani Umayyah, kwani  Imam AS alikuwa akibainisha kinagaubaga suala la Uimamu, kuwa ni  mfumo wa utawala wa Kiislamu na uongozi kwa jamii ya Kiislamu. Kwa kutumia njia hiyohiyo, Imam Sajjad AS alikuwa akiwaeleza watu kile kinachojiri kwenye jamii ya Kiislamu na hasa kuhusiana na  tawala zilizokuwa zikitumia  mabavu, zilizojaa ufasiki na unafiki kama vile utawala wa Yazid na Abdul Malik Marwan ambazo hazikutawala kwa mujibu wa misingi na sheria za  Kiislamu.

Abu Hamza Thumali mmoja kati ya wafuasi na wasaidizi wa karibu wa Imam Sajjad AS amenukuliwa akisema kwamba, Imam AS alikuwa akiwausia wafuasi wake na waumini wengine wajiweke mbali na maliwazo na faraja za uwongo walizopewa na watawala madhalimu. Imam Sajjad alikuwa akiwatahadharisha wafuasi wake dhidi ya kushirikiana na watawala dhalimu na kuwaambia kwamba walikuwa wakiwahadaa kwa anasa na vivutio hivyo bandia vya kidunia ili kudhoofisha imani zao na wakati huohuo kupunguza makali ya upinzani wao dhidi ya mfumo wa utawala wa Bani Umayyah. Imam alikuwa akisema: 'Enyi waumini! Mataghuti ni watu walioikumbatia dunia, nyoyo zao zimezama kwenye ulimwengu huu, hivyo msihadaike na neema zisizokuwa na thamani na zenye ladha ya muda mfupi tu.' Imam Sajjad alikuwa akiwataka wafuasi wake wajifunge kibwebwe katika kukabiliana na vitendo vya dhulma na ukandamizaji na kuwakumbusha misukosuko na mashinikizo makubwa  waliyoyapata wafuasi wa Ahlul Bayt katika zama za Muawiya, Yazid na Marwan. Katika lahdha kama hizo , Imam pia alikuwa akielezea suala la Uimamu na kubainisha ni  mtu gani aliyepaswa kufuatwa baada ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na ili kuondoa shaka na wasiwasi kwenye nyoyo na fikra za wafuasi wake na hadhirina alikuwa akisema; 'Tangulizeni na wekeni mbele amri ya Mwenyezi Mungu ya kumtii mtu ambaye Mwenyezi Mungu amelazimisha atiiwe, na kamwe msiwatangulize mataghuti ambao wamepumbazika na kuikumbatia dunia'.

 

Dua ni moja kati ya mbinu za kimahubiri zilizokuwa zikitumiwa na Imam Sajjad AS katika zama zake. Shakhsia huyo mkubwa alikuwa akibainisha masuala mbalimbali kama vile ya kielimu, maarifa ya Kiislamu, kiirfani, kijamii, kimalezi na masuala nyeti ya kisiasa katika sura ya dua, ambapo dua zake nyingi zimekusanywa kwenye kitabu kinachoitwa Swahiifat Sajjadiyyah. Katika kitabu hicho ambacho kinajulikana kwa jina la 'Injili ya Ahlul Bayt' na 'Zaburi ya Watu wa Muhammad', Imam Sajjad  kwa kutumia njia ya dua ameweka vigezo mbalimbali vya maisha ya Kiislamu kwenye fikra za watu. Imam Ali Zainul Abidiin  AS akiwa na uoni wa mbali katika zama  hizo ambazo  watu wake walio wengi walikuwa wamepumbazika na dunia na kuyapa mgongo masuala ya ibada na mafundisho ya Kiislamu, alitumia dua kama njia ya kuwaamsha na kuwaongoza kwenye njia ya kumuabudu Allah SW na kufuata umaanawi. Jambo la kuzingatiwa hapa ni hili kwamba, Imam AS kwa kutumia dua aliweza kubainisha wazi masuala ya Uimamu na ukweli wa Ahlul Bayt AS katika kadhia ya kuchukua uongozi wa jamii ya Kiislamu. Miongoni mwa mbinu zilizotumiwa na Imam Sajjad AS za kuweka wazi zaidi nafasi ya Ahul Bayt AS, ilikuwa ni suala la kukaririwa kwenye dua zake utajo huu wa kumswalia Mtume na Aali zake watoharifu kwa kusema 'Rehema na amani za Allah ziwe kwa Mtume Muhammad na Ahli wa Muhammad'.

Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu maalumu ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS kimefikia ukingoni. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani, na hasa wafuasi wa kweli wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad SAW, kwa mnasaba huu adhimu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

Tags