Oct 15, 2018 10:28 UTC

Miongoni mwa maswala yanayoulizwa kuhusu harakati ya Imam Hussein bin Ali (as) na tukio la Ashura ni kwamba, je, yote tunayoyasikia hii leo kuhusu tukio hilo la mauaji ya Imam Hussein na masabaha zake katika medani ya Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria ni sahihi, au kuna uwezekano baadhi yamepotoshwa?

Tukio la Ashuraa huko Karbala ni miongoni mwa matukio yasiyo na kifani katika historia ya Uislamu na kutokana na kuwepo nyaraka na ushahidi mwingi wa kihistoria linatambuliwa kuwa na miongoni mwa matukio yenye mapokezi sahihi na yaliyoeleza kwa kina mambo mengi yaliyojiri siku hiyo, sababu na malengo yake. Hata hivyo ukweli huu hauzuia kujitokeza swali kwamba je, baadhi ya matukio ya siku hiyo hayajapotoshwa?   

Kupotosha au "Tahrif" kwa lugha ya Kiarabu, kuna maana ya kubadili, kugeuza na kupeleka kitu kusiko. Kwa maneno mengine ni kuwa, tahrif ina maana ya kubadilisha neno au sentensi au tukio kwa njia na sura ambayo itatoa maana tofauti kabisa na ile ya asili. Kufanya tahrif na upotoshaji kuhusiana na watu adhimu ambao kauli na matendo yao huwa ni kigezo na ruwaza njema kwa wanadamu au kuhusiana na matukio yanayoakisi nafasi na mchango wao ni jambo hatari sana na lenye athari mbaya. Kwa mfano tu tahrif na upotoshaji uliofanyika katika mafundisho ya Mitume waliokuja kabla ya Mtume wa Mwisho, Muhammad (saw) hadi sasa bado unasababisha makosa makubwa sana baina ya wanadamu na katika ufahamu wao wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu na ni vigumu sana kuweza kuepuka athari na mtokeo yake mabaya.

Upotoshaji unaweza kufanyika kwa sura mbili za kidhahiri na kimaana. Upotoshaji wa kidhahiri una maana ya kukata sentensi ya maelezo ya asili ya tukio fulani au kuzidisha sentensi ambayo hatimaye hutoa maana isiyokuwa ya asili na iliyokusudiwa na msemaji. Katika matukio ya kihistoria pia yumkini kukafanyika upotoshaji wa aina hii wa kidhahiri na kisura kwa maana ya kuficha na kutoeleza sehemu asili ya tukio makhsusi na badala yake kupachika na kusimulia tukio jingine ambalo halikutukia katika historia mahala pake. Kuondoa na kupachika huku kwa matukio ya asili na yasiyo ya asili hupotosha sura halisi na ya asili ya tukio husika na hatimaye kulikosesha thamani tukio hilo na taathira zake katika historia ya mwanadamu. 

Upotoshaji wa kimaana una maana ya kubadili na kupotosha sababu halisi za tukio hilo, malengo na matokeo yake na mwishowe maana ya tukio hilo hubadilika kabisa na kupata sura nyingine katika fikra za msikilizaji.     

Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, maana zote mbili za upotoshaji wa kidhahiri na kimaana zinaonekana katika baadhi ya matukio ya siku ya Ashuraa kama ilivyo katika matukio mengine mengi ya kihistoria. Upotoshaji huo umefanywa na makundi mbalimbali na kwa sababu tofauti. Baadhi ya upotoshaji huo umefanywa na unafanywa na maadui wa harakati hiyo ya mageuzi na marekebisho ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as). Kwa mfano tu tangu hapo mwanzoni, maadui walifanya jitihada za kupotosha sababu na malengo ya harakati ya Imam na kuitaja kuwa ilikusudia kuzusha hitilafu katika Umma na kwamba ni aina fulani ya uasi dhidi ya utawala wa zama hizo. Madai haya yalipingana moja kwa moja na lengo halisi la Imam Hussein ambalo alilitangaza waziwazi mwanzoni mwa harakati yake kuwa ni kufanya marekebisho katika Umma wa babu yake, kupambana na uzushi na upotoshaji uliokuwa umefanyika katika dini ya Uislamu. Upotoshaji mwingine wa aina hii wa tukio la Ashuraa ni madai kuwa vita vya siku ya Ashuraa mwaka 61 Hijria vilikuwa vita ya kugombea madaraka kati ya Imam Hussein (as) na Yazid bin Muawiya na kwamba hatimaye Imam Hussein alishindwa vita hiyo. Madai haya hayakubaliwi na mwanahistoria yeyote wa Kiislamu bali ushahidi mwingi wa kihistoria unayakana na kuyakadhibisha. Upotoshaji huu unatambuliwa kuwa ni wa kimaana kwa maana ya kupotosha sababu, lengo na matokeo ya harakati ya Imam Hussein (as) siku ya Ashuraa mwaka 61 Hijria.

Baadhi ya upotoshaji wa tukio la Ashuraa sawa kabisa na inavyoshuhudiwa katika historia ya mataifa na dini nyingine, umesababishwa na tabia ya baadhi ya wanadamu ya kutaka kutengeneza mashujaa na kubuni ngano. Kwa maana kwamba, wapo baadhi ya watu waliotaka kukuza kupita kiasi sifa na nguvu za mashujaa wao wa kitaifa au kidini mbele ya watu wa kaumu, taifa au dini nyingine. Mfano wa upotoshaji huu ni kama ule unaodai kwamba, jeshi la Yazid lililokuwa likiongozwa na Umar bin Sa'ad lilikuwa na wapiganaji milioni moja na laki sita na kwamba Imam Hussein peke yake aliua wanajeshi elfu 24 kati yao! Mfano mwingine wa upotoshaji wa aina hii ni ule unaotaja sifa na uwezo wa kimwili wa masahaba wa Imam Hussein katika medani ya Karabala ambazo hazioani na akili wala mantiki.

Ukweli ni kwamba, masahaba wa Imam Hussein japokuwa walikuwa mashujaa wa kupigiwa mfano, wapiganaji hodari, jasiri na imara lakini walikuwa wanadamu wa kawaida ambao imani yao kubwa ya Uislamu, utakasifu wa nyoyo zao, ikhlasi, amali na matendo yao mema na kumtambua ipasavyo Imam na kiongozi wao viliwapa ari, moyo thabiti na ushujaa wa aina yake na kuwasaidia kutengeneza hamasa iliyobakia hai katika historia ya mwanadamu. Thamani ya Ashuraa pia inatokana na vigezo hivyo ambavyo vinaweza kutumiwa na kila mwanadamu mwenye imani, ikhlasi na moyo safi wakati wa mashaka makubwa kwa ajili ya kupata saada ya milele. 

Upotoshaji mwingine ambao kidhahiri unaonekana ni wa kimaana ni ule wa baadhi ya watu kutaka kuhamasisha majlisi na vikao vya maombolezo ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein na masahaba zake kwa kutumia mambo yaliyotajwa kwenye vyanzo visivyokuwa vya kuaminika, kufanya mambo yasiyooana na mafundisho ya dini na wakati mwingine kuzusha na kubuni visa na matukio wao wenyewe. Inashuhudiwa kuwa, mara nyingi mambo kama haya badala ya kuhudumia malengo ya harakati ya Imam Hussein (as) hudhoofisha harakati hiyo na kuchafua sura ya mafundisho halisi ya Uislamu. Miongoni mwa upotoshaji huu ni visa vinavyotajwa katika baadhi ya majlisi kama kile cha harusi ya Qasim mwana wa Imam Hassan (as) na mmoja kati ya mabinti wa Imam Hussein (as) siku ya Ashuraa na katika kilele cha mashaka na misukosuko ya vita, ngano kwamba siku hiyo ya Ashuraa ilirefushwa kwa masaa sabibi na mbili, madai kwamba Bibi Laila mke wa Imam Hussein (as) na mama wa mwanaye, Ali al Akbar (as) alikuwepo Karbala na kadhalika ambavyo vyote havikupokewa katika vitabu vya historia vya kuaminika.

Miongoni mwa vyanzo vikuu vya ngazo nyingi zinazotumiwa kupotosha matukio ya siku ya Ashuraa na mapambano ya Imam Hussein (as) ni kitabu cha "Raudhatu Shuhadaa" kilichoandikwa na mtu anayejulikana kwa jina la Mulla Hussein Kashifi. Bwana huyu alikuwa miongoni mwa mahatibu na waandishi wa eneo la Herat katika Afghanistan ya sasa ambaye aliishi mwishoni mwa karne ya 9 na mwanzoni mwa karne ya 10 Hijria. Kwa bahati mbaya kitabu hicho kilienea kwa wingi na kupata ushawishi katika majlisi za maombolezo ya Ashuraa na inasikitisha kuona kwamba, kimejaa ngano na visa vingi vya kubuni. Kitabu cha Asrarul Shahada kilichoandikwa na Mulla Agha Darbandi katika karne ya 19 pia ni miongoni mwa vitabu vilivyojaa upotoshaji na hurafa nyingi kuhusiana na harakari ya Imam Hussein na masahaba zake na mapambano yao huko Karbala.

Miaka iliyofuata na hata kabla yake wanazuoni wengi wa Kiislamu waliandika vitabu vingi vilivyokosoa upotoshaji huo na kusimulia kisa na matukio ya Karbala na Ashuraa kutoka kwenye marejeo sahihi na asili ya historia ya Uislamu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni kile kilichoandikwa na Ayatulla Murtadhaa Mutahhari na kukipa jina la Hamasa ya Imam Hussein (as). Pamoja na hayo yote inatupasa kusisitiza kuwa, matukio ya Ashuraa na mapambano ya Imam Hussein huko Karbala ni miongoni mwa matukio ambayo yamesajiliwa kwa umakini mkubwa na kuandikwa katika vitabu mashuhuri vya wanazuoni wa Kiislamu kama Tabari katika kitabu chake cha Tarikhul Umami Walmuluuk, Al Kaamil fi Tariikh cha Ibn al-Athir, Murujudh Dhahab cha al Masu'di, al Bidaya Wannihayah cha Ibn Kathiri na kadhalika.          

Tags