Sheikh Zakzaky na dhulma za kimyakimya dhidi ya Waislamu wa Nigeria
(last modified Mon, 13 Jan 2020 13:56:06 GMT )
Jan 13, 2020 13:56 UTC
  • Sheikh Zakzaky na dhulma za kimyakimya dhidi ya Waislamu wa Nigeria

Nigeria ina historia ya ukandamizaji wa harakati za Kiislamu. Ukatili, mauaji na ukandamizaji wa harakati za Kiislamu nchini Nigeria vilishadidi zaidi mwaka 2011.

Kuanzia wakati huo jeshi la serikali ya Nigeria inayoungwa mkono na kusaidiwa na tawala za kibeberu kama Marekani, Israel na kibaraka wao, Saudi Arabia, imekuwa ikitekeleza mpango kabambe wa kuzima na kukandamiza harakati zote hai za Kiislamu kwa kutumia sababu mbalimbali hususan harakati zinazofuata mafundisho ya Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw).

Hivi sasa imepita zaidi ya miaka minne tangu jeshi la Nigeria lilipofanya mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu katika mji wa Zaria. Tarehe 12 ya mwezi Disemba mwaka 2015 jeshi la Nigeria liliwaua shahidi Waislamu zaidi ya elfu moja wa madhehebu ya Shia katika mji huo. Mkasa wa kusikitisha wa mauaji hayo ulianza wakati vijana wa Kiislamu wa Nigeria walipokuwa katika maandalizi ya shughuli za maombolezo na kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Ali bin Musa al Ridha katika kituo cha kidini cha Baqiyyatullah mjini Zaria. Ghafla vijana hao walijikuta katika hujuma kubwa na ya kinyama ya jeshi la Nigeria. Katika shambulizi hilo idadi kubwa ya Waislamu waliuawa shahidi wakiwemo wasaidizi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) kama Sheikh Muhammad Nour, Dakta Mustafa Said na Ibrahim Othman. Baada ya mauaji hayo jeshi la Nigeria lilichoma moto kituo hicho cha kidini. Jeshi hilo halikutosheka na mauaji na ukatili huo. Siku iliyofuatia jeshi la Nigeria lilishambulia nyumba ya Sheikh Zakzaky na kuwaua kwa umati Waislamu wengi waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya kumhami kiongozi wao bila ya kuwa na silaha ya aina yoyote. Waislamu hao walikuwa wamejitolea kumhami kiongozi wao ambaye anasifika kwa kuamiliana nao kwa upendo na hakuruhusu walinzi wake kushika silaha ya aina yoyote. Awali jeshi la Nigeria lilichoma moto nyumba ya Sheikh Zakzaky na kushambulia watu waliokuwa wakitoka ndani ya nyumba hiyo na kuwaua kwa umati. Sheikh Zakzaky na mkewe walijeruhiwa kwa kupigwa risasi.

Sheikh Zakzaky alijeruuhiwa vibaya kwa risasi

Watoto watatu wa kiume wa Sheikh Ibrahim Zakzaky waliuawa shahidi katika shambulizi hilo. Mwaka mmoja kabla yake pia watoto wengine watatu wa kiongozi huyo wa Waislamu wa Nigeria walikuwa wameuawa kwa kupigwa risasi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Binti wa kiongozi huyo pia alikamatwa na kudhalilishwa, na dada mkubwa wa Sheikh Zakzaky akauawa shahidi. Mwanamke mwingine aliyekuwa mja mzito aliavya mimba yake papo hapo na akafa shahidi baadaye kutokana na mateso na manyanyaso ya jeshi la Nigeria. Sheikh Zakzaky na mke wake walikamatwa na kupelekwa kusikojulikana. Haya yote yalifanyika licha ya katiba ya Nigeria kudhamini uhuru wa kufanya ibada na mikusanyiko ya kidini.  

Hapa kunajitokeza maswali kwamba, ni kwa nini Waislamu hao ambao hawakuwa na silaha, hawakufanya uharibifu wa aina yoyote na walikusanyika tu kwenye kituo cha kidini kwa shughuli za kidini, wakauawa bila dhambi yoyote? Ni kwa nini Sheikh Ibrahim Zakzaky anayejulikana kwa maadili yake mema na kwa kutumia mbinu za amani na kujiepusha na ghasia na utumiaji mabavu katika harakati zake za kidini, anaendelea kuteswa na kukandamizwa katika jela za Nigeria?

Maswali haya na mengine mengi yanayohusiana na jinai na dhulma zinazofanyika dhidi ya Waislamu wa Nigeria bado hayajapatiwa majibu. Duru za kimataifa ambazo aghlabu zimekuwa zikinyamazia kimya dhulma zinazofanywa dhidi ya Waislamu au kuchuja na kuficha habari za dhulma na maafa yanayowasibu, hadi sasa hazijachuka hatua yoyote ya maana mkabala wa ukatili unaofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, ni watetezi kadhaa tu wa haki za binadamu ndio waliosimama tarehe 15 Disemba mwaka huo wa 2015 na kulituhumu jeshi la Nigeria kuwa limefanya mauaji ya mamia ya watu katika mji wa Zaria. Ripoti ya watetezi hao wa haki za binadamu ilisema kuwa, ukatili huo uliotoa roho za watu waliokaribia elfu moja ni "mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu." 

Mamia ya Waislamu waliuawa katika shambulizi la jeshi la Nigeria dhidi ya nyumba ya Sheikh Zakzaky mwaka 2015

Akisimulia jinsi mauaji hayo yalivyotokea katika kongamano la kumbukumbu ya kutimia miaka minne tangu baada ya mauaji ya Zaria lililofanyika hapa mjini Tehran, binti wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Suhaila Zakzaky anasema: "Miaka minne iliyopita jeshi la Nigeria liliwaua kinyama watu zaidi ya elfu mmoja ambao hawakuwa na hatia yoyote wakiwemo wanawake 297 ambao 23 miongoni mwao walikuwa wajawazito, wanaume 548 na watoto 193. Familia 39 ziliangamizwa kikamilifu katika mauaji ya Zaria. Wanajeshi hao pia walifanya ukatili mkubwa ikiwa ni pamoja na kuchoma moto majengo na watu waliokuwamo. Hawakuhurumia hata vitoto vichanga."

Suhaila Zakzaky anaendelea kusimulia kwamba: "Unyama huo wote ulifanyika kwa madai kwamba, ni jibu kwa njama eti ya jaribio la kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi, lakini sasa inaeleweka wazi kuwa, ukatili huo ni njama iliyokuwa imepangwa kwa ajili ya kumuua Sheikh Zakzaky na wafuasi wake ili kuangamiza kabisa Harakari ya Kiislamu nchini Nigeria."

Suhaila Zakzaky

Suhaila anasema, baada ya tukio hilo Sheikh Zakzaky na mke wake Malama Zinat na wanaharakati wengine wa harakati ya IMN walitiwa nguvuni na wanaendelea kushikiliwa na vyombo vya dola.

Itakumbukwa kwamba, mwaka 2016 Mahakama Kuu ya Nigeria iliitaka serikali ya nchi hiyo imwachie huru Sheikh Zakzaky lakini jeshi la nchi hilo limekataa kutii amri hiyo.

Kuhusu hali ya kiafya ya baba na mama yake, Suhaila Zakzaky anasema: Hali ya kiafya ya baba na mama yangu inazidi kuwa mbaya siku baada ya nyingine kutokana na majeraha ya risasi walizopigwa katika shambulizi la Zaria. Hadi sasa Sheikh amepatwa na kiharusi mara kadhaa na mama yangu hawezi kutembea vizuri kutokana na masaibu mengi anayokutana nayo huko jela. Hivi karibuni pia imegunduliwa kwamba Sheikh anasumbuliwa na sumu kali mwilini mwake."   

Suhaila Zakzaky

Chanzo na sababu kuu ya uadui wa jeshi na serikali ya Nigeria dhidi ya Sheikh Zakzaky na harakati yake ya Kiislamu ni kwamba wanaitambua harakati hiyo ya Islamic Movement of Nigeria (IMN), kuwa ni harakati ya kisiasa. Nchi ya Nigeria ndiyo yenye jamii kubwa zaidi ya watu barani Afrika na ya kumi duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu. Zaidi ya asilimia 50 ya watu zaidi ya milioni 170 wa Nigeria ni Waislamu. Vilevile kutokana na kuongezeka kwa kasi jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo, Marekani, Israel na Saudi Arabia zimekuwa zikiitisha serikali ya Abuja kuhusiana na kile zinachodai ni 'mapinduzi ya Mashia' na zinakabiliana na jamii ya Waislamu hao kwa kufadhili makundi ya kigaidi kama Boko Haram. Mauaji ya Waislamu hao yalianza kushika kasi mwaka 2011. Serikali ya Nigeria ikisaidiwa na tawala za Marekani, Israel na utawala wa Saudia walilifadhili kundi la kigaidi la Boko Haram lenye mielekeo ya kiwahabi na kuanza kufanya mauaji ya holela dhidi ya Wislamu wasiokubaliana na mitazamo yao hususan wa madhehebu ya Shia. Waislamu wa madhehebu hiyo walianza kukamatwa, kuteswa na kufungwa jela kwa shabaha ya kusitisha kasi ya harakati za kidini za Waislamu hao. Mwenendo huo uliendelea na kufikia kileleni katika mauaji ya kutisha ya mwaka 2015 katika mji wa Zaria.

Kuendelea kushikiliwa gerezani Sheikh Zakzaky pia ni njama iliyopangwa awali na Marekani, Israel na Saudi Arabia kwa ajili ya kuangamiza kabisa harakati ya IMN. Tawala hizi zina wasiwasi kuhusiana na kupanuka shughuli za kidini za harakati hiyo hadi kwenye nchi za kandokando ya Nigeria na kwa msingi huo zimekhitari kutumia mbinu za kikatili na mauaji kuzuia harakati hiyo. Harakati ya IMN ni jumuiya inayojihusisha na masuala ya kidini na kueneza maarifa ya Uislamu; na katika upande wa kisiasa inapinga vikali utawala wa Kizayuni wa Israel na dhulma zinazofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina. Ni kwa sababu hiyo pia ndiyo maana mwaka 2014 jeshi la Nigeria lilivamia maandamano ya amani ya wafuasi wa harakati hiyo ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds na kuua Waislamu 33 miongoni mwao wakiwemo watototo watatu wa Sheikh Zakzaky.

Mwaka 2015 wakati Sheikh Ibrahim Zakzaky alipoiandikia barua serikali kuu ya Nigeria akiishauri ikate uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mauaji yake dhidi ya watu wa Palestina, serikali ya Abuja ilijibu barua hiyo kwa kutoa roho za Waislamu karibu elfu moja katika mji wa Zaria na kuvunja kituo cha kidini cha Baqiyatullah. Baada ya kuandika barua hiyo Sheikh Zakzaky aliwaambia waandishi wa habari kwamba: "Serikali Kuu ya Abuja ni mwana wa nchi za Magharibi zenye kiu ya mafuta ya Nigeria."

Sheikh Ibrahim Zakzaky

Kwa sasa Sheikh Zakzaky na mkewe wanaendelea kusota katika jela la Nigeria huku jumuiya za kimataifa za eti kutetea haki za binadamu zikiendelea kukaa kimya. Hata hivyo ukweli ni kwamba, hata kama mwanaharakati huo atauawa akiwa jela au baadaye, harakati ya kupigania haki na kueneza mafundisho ya kweli itaendelea siku na nyakati zote….