Misri: Tuna hamu ya kuwa na uhusiano chanya na Iran
(last modified Thu, 20 Jul 2023 03:42:52 GMT )
Jul 20, 2023 03:42 UTC
  • Misri: Tuna hamu ya kuwa na uhusiano chanya na Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ameitaja Iran kama nchi kubwa na yenye ushawishi katika eneo na kusisitiza kuwa, maingiliano baina ya nchi mbili hizi hayajawahi kuvunjika.

Ahmed Abu-Zeid ameiambia kanali ya CBC News kuwa, Misri ina hamu ya kuwa na uhusiano chanya na Iran na kwamba hakuna wakati wowote mawasiliano baina ya nchi mbili hizi umekatika.

Abu-Zeid ambaye amenukuliwa pia na shirika la habari la IRNA ameeleza kuwa, nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika inataka kuona hali ya uthabiti inatawala katika eneo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri  amekumbusha kuwa, viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo wametangaza mara kadhaa kuwa wako tayari kuanza mazungumzo rasmi na ya haraka baina yao na wenzao wa Iran.

Mwanadiplomasia huyo wa Misri amesema, pande mbili za Iran na Misri zimeonesha hamu ya kustawisha uhusiano baina yao kulingana na mabadiliko yaliyotokea hivi karibuni kwenye ukanda huu.

Tovuti ya habari ya Al-Arabi Al-Jadeed hivi karibuni iliwanukuu wanadiplomasia wa Misri wakisema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Misri zimefikia hatua nzuri ya kukurubisha pamoja mitazamo yao hususan katika masuala yanayohusiana na maeneo yao.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian alisema Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha kuimarisha uhusiano na nchi zote za Kiislamu ikiwemo Misri. Aidha alionya dhidi ya njama za maadui wa umma wa Kiislamu wanaotaka kuibua mifarakano na migawanyiko miongoni mwa mataifa ya Kiislamu.