Libya, familia za wahanga waliozikwa kwenye makaburi ya umati zataka wahusika wanyongwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101062
Familia za watu waliouawa na kuzikwa kwenye makaburi ya halaiki zimepinga adhabu ya vifungo vya jela kwa wale waliohusika na mauaji ya mamia ya raia na kuzikwa kwenye makaburi hayi katika mji wa Tarhuna, kusini mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli, na badala yake zinataka wapewe adhabu ya kifo
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 14, 2023 12:21 UTC
  • Libya, familia za wahanga waliozikwa kwenye makaburi ya umati zataka wahusika wanyongwe

Familia za watu waliouawa na kuzikwa kwenye makaburi ya halaiki zimepinga adhabu ya vifungo vya jela kwa wale waliohusika na mauaji ya mamia ya raia na kuzikwa kwenye makaburi hayi katika mji wa Tarhuna, kusini mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli, na badala yake zinataka wapewe adhabu ya kifo

Musab Abu Kleish, mjumbe wa shirika la "Families of Victims of Tarhuna", anaeleza kuwa familia zote za wahanga wa makaburi ya halaiki haziridhishwi na hukumu za jela dhidi ya washtakiwa, "kwa sababu wamehusika moja kwa moja na mauaji ya mamia ya raia."

Abu Kleish anasema kuwa familia za wahanga hao zina madai makuu matatu, kwanza ni kutambua maiti za waliosalia, pili kuwaandama wahalifu waliohusika na jinai hiyo na kutoa hukumu kali dhidi yao, na la tatu ni kuzifidia familia za wahanga.

Makaburi ya kwanza ya halaiki yalipatikana Tarhuna, umbali wa kilomita 80 kusini mwa mji mkuu, Tripoli, mnamo Juni 2020, baada ya vikosi vya Jenerali mstaafu Khalifa Haftar kuondoka eneo hilo.

Makaburi ya halaiki ya Tarhuna

Muhammad al-Lafi, baba yake Murad (30), ambaye alipatikana kwenye kaburi la halaiki, amesema akiwa amekumbatia picha ya mtoto wake kwa uchungu mwingi, kwamba wanamgambo wa al-Kani walimteka nyara mwanaye mnamo 2019 huko Tarhuna, kisha akauawa na mwili wake ukafichwa kwenye kaburi la halaiki, kabla ya kutambuliwa akiwa pamoja na makumi ya watu wengine mapema 2022.

Al-Lafi anaamini kuwa, adhabu ya kifo ndiyo hukumu pekee inayoweza kupunguza huzuni za familia za wahanga wa ukatili huo baada ya kumpoteza mtoto wake wa kiume ambaye anasema aliuawa kwa "damu baridi," licha ya kwamba hakujihusisha katika migogoro ya kisiasa.

Itakumbukwa kuwa, mwezi Februari mwaka jana, mahakama ya kijeshi mjini Tripoli ilitoa hukumu za vifungo vya kuanzia miaka 6 10, 15 au kifungo cha maisha jela kwa karibu watuhumiwa 30 wa mauaji ya mamia ya raia waliopatikana kwenye makaburi ya halaiki ya Tarhuna.

Hukumu mpya zinatarajiwa kutolewa dhidi ya makumi ya washtakiwa wengine katika wiki zijazo, kulingana na chanzo katika Wizara ya Sheria ya Libya.