Aug 30, 2023 02:31 UTC
  • Kundi la al-Shabaab ladhibiti miji mitano katikati ya Somalia

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameripotiwa kuteka miji mitano iliyoko katikati ya Somalia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, magaidi hao wakufurishaji wametwaa miji ya Wabho, Osweyne, Budbud, Gal’ad, na Masagaway katika jimbo la Galmudug, baada ya wanajeshi wa Somalia kuondoka katika miji hiyo juzi Jumatatu.

Habari zaidi zinasema, genge hilo la kigaidi limeua wanajeshi 178 wa Somalia katika mapigano baina ya pande mbili hizo katikati ya Somalia. Hata hivyo halijasema idadi ya wanachama waliouawa katika makabiliano hayo.

Huku hayo yakijiri, Vikosi Maalumu vya Danab vya jeshi la Somalia vimeua makumi ya magaidi wa al-Shabaab katika operesheni ya hivi punde katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Arab Dheeq Ahmed, Kamanda wa Kikosi cha 5 cha Vikosi vya Danab amesema magaidi zaidi a 47 wa al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni hiyo mpya iliyolenga maficho yao katika eneo la Yaq Dabey, jimbo la Lower Juba.

Wanajeshi wa Somalia

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, magaidi zaidi ya 3,000 wameuawa katika awamu ya kwanza ya operesheni za kulitokomeza kundi hilo hasa katika majimbo la Hirshabelle na Galmadug.

Hivi karibuni, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia alisema lengo la operesheni za kijeshi zinazoendelea nchini humo ni kulitokomeza na kulisambaratisha kundi la kigaidi la al-Shabaab katika kipindi cha miezi mitano ijayo.

Somalia imekuwa katika vita na mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shaabab lilioasisiwa mwanzoni mwaka mwaka 2004, na ambalo limetangaza kuwa na mfungamano na mtandao wa al-Qaeda.

Tags