UN: Wahajiri 400 wameaga dunia kwa mafuriko Libya
(last modified Wed, 20 Sep 2023 07:17:58 GMT )
Sep 20, 2023 07:17 UTC
  • UN: Wahajiri 400 wameaga dunia kwa mafuriko Libya

Umoja wa Mataifa umesema mamia ya wahajiri ni miongoni mwa maelfu ya watu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na kimbunga huko mashariki mwa Libya.

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema hayo jana Jumanne katika ripoti yake na kuongeza kuwa, wahajiri 400 waliaga dunia kwa mafuriko wiki iliyopita mashariki ya Libya.

Ripoti hiyo imenukuu Shiriki la Afya Duniani (WHO) iliyosema kuwa, mpaka sasa watu 4000 wamethibitishwa kuaga dunia mashariki ya Libya kutoka na mafuriko hayo, wakiwemo wahajiri 400.

Hata hivyo hadi sasa zaidi ya watu 11,000 wamethibitishwa kufariki dunia na wengine 10,000 hawajulikani walipo. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali ya Libya. 

Kuna maelfu ya wahajiri wa Kiafrika na wengine kutoka Mashariki ya Kati wanaoshi katika kambi za wakimbizi nchini Libya, aghalabu yao wakiwa na hamu ya kwenda Ulaya kusaka maisha.

Wahajiri Libya

Tarehe 10 mwezi huu wa Septemba, kimbunga cha Daniel kilisababisha mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini Libya katika miongo kadhaa iliyopita.

Serikali ya Libya imetangaza hali ya dharura ya mwaka mzima kwa shabaha ya kuzuia kuenea magonjwa ya kuambukiza katika maeneo yaliyokuumbwa na mafuriko hayo mashariki mwa nchi hiyo.