Makumi ya wakimbizi wakufa njaa Gambella, Ethiopia
(last modified Fri, 22 Sep 2023 02:43:47 GMT )
Sep 22, 2023 02:43 UTC
  • Makumi ya wakimbizi wakufa njaa Gambella, Ethiopia

Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC) imesema wakimbizi zaidi ya 30 wamepoteza maisha kutokana na njaa na utapiamlo katika jimbo la Gambella lililoko magharibi ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Taarifa ya tume hiyo imesema jimbo hilo lina wakimbizi zaidi ya laki nne (400,000), ikisisitiza kuwa kuna udharura wa kuendelea kutuma misaada ya kibinadamu kwa jamii za wakimbizi katika eneo hilo.

Baadhi ya kambi za wakimbizi katika jimbo hilo hazijapokea misaada tokea mwezi Mei mwaka huu, huku nyingine zikikosa kufikiwa na misaada hiyo tangu mwezi wa Juni.

"Wakimbizi hao waliaga dunia kutokana na njaa na utapiamlo, huku wengine wakipoteza maisha baada ya kushambuliwa walipoondoka kambini kwenda kutafuta chakula," imeeleza taarifa ya EHRC. 

Wanamgambo katika jimbo la Gambella

Aidha Idara ya Wakimbizi na Wahamiaji ya Serikali ya Federali ya Ethiopia (RRS) iliripoti karibuni pia kwamba, vifo vinavyotokana na njaa vimenakiliwa katika kambi za wakimbizi za Gambella, baada ya kusimamishwa utoaji wa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo tokea mwezi Mei.

Taasisi hiyo ya kushughulikiwa wakimbizi ya serikali ya Ethiopia imebainisha kuwa, mashambulizi ya silaha katika eneo la Amhara yaliyoshtadi tokea Agosti mwaka huu na pia kuendelea kuwasili wakimbizi katika majimbo ya Amhara, Benishangul-Gumuz, Gambella na Somali, wakitokea nchi jirani, kumechangia kuongezeka hitaji la misaada ya kibinadamu katika maeneo hayo.