Oct 07, 2023 07:26 UTC
  • Wananchi wa Morocco waandamana kupinga uhusiano wa kawaida na Israel

Kwa mara nyingine tena, wananchi wa Morocco wamefanya maandamano ya kupinga hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel; uhusiano ambao kwa sasa umefikisha mwaka mmoja.

Waandamanaji hao walisikika pia wakipiga nara za kulaani mashambulio ya kinyama ya jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina, na wakatii huo huo kutangaza kuwa pamoja na wananchi hao wa Palestina.

Wananchi wa Morocco walioshiriki maandamano hayo ya jana Ijumaa mjini Rabat huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina, walitangaza kuwa wanapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel kwa namna yoyote ile.

Desemba 2020, Morocco na utawala haramu wa Israel zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kwa ushawishi wa Marekani. Na kama sehemu ya makubaliano hayo, Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alikubali kutambua mamlaka ya Morocco juu ya Sahara Magharibi. Hata hivyo serikali ya rais wa sasa wa nchi hiyo Joe Biden imesema itauangalia upya uamuzi huo.

Wananchi wa Morocco hadi sasa wameshaandamana na kumiminika mabarabarani mara kadhaa sambamba na kuzichoma moto bendera za utawala haramu wa Kizayuni, kuonyesha upinzani wao dhidi ya hatua ya serikali ya Rabat kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv na kutaka uhusiano huo ukomeshwe.

Kadhalika Wamorocco wametumia jukwaa hilo la maandamano kulaani kushtadi hatua ya wanajeshi wa utawala haramu wa Israel ya kuwashambulia waumini wa Kipalestina, huku mamia ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali wakiingia kwa mabavu katika eneo la Msikiti wa al-Aqsa huko Quds (Jerusalem) Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Tags