Salva Kiir kuwa mwenyeji wa viongozi wa Sudan kujadili amani
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir amesema karibuni hivi atakuwa mwenyeji wa mkutano utakaowaleta pamoja viongozi wa pande mbili zinazopigana nchini Sudan, yaani Jeshi la Taifa la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF)
Taarifa kutoka Idara ya Habari ya Rais Kiir imeeleza kuwa, mkutano huo utafanyika wiki ijayo. Hata hivyo taarifa hiyo haijaeleza ni viongozi gani watashiriki kwenye mkutano huo wa kujadili amani ya Sudan.
Rais Kiir jana Jumatatu baada ya kufanya mazungumzo juu ya hali ya Sudan na Malik Agar Eyre, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Sudan, alitoa mwito kwa viongozi wa kisiasa katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika kusitisha mgogoro unaoendelea kushuhudiwa kupitia njia za mazungumzo na amani.
Hii ni katika hali ambayo, usuluhishi wa kieneo na kimataifa uliofanywa huko nyuma kwa madhumuni ya kuhitimisha mapigano hayo na kuzikutanisha pande mbili kwenye meza ya mazungumzo haujazaa matunda hadi sasa.

Mapigano nchini Sudan yaliyozuka Aprili 15 mwaka huu mbali na kuuawa maelfu ya watu, lakini pia yamesababisha wimbi kubwa la watu kukimbilia nchi jirani ikiwemo Sudan Kusini. Jumapili ya juzi, mgogoro huo ulitimiza miezi sita.
Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Rais Salva Kiir alikutana na mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa jijini Pretoria na kufanya mazungumzo kuhusu mzozo unaoendelea nchini Sudan pamoja na mchakato wa amani nchini mwake.