Nov 16, 2023 12:49 UTC
  • Bunge la Kenya laidhinisha mpango wa nchi hiyo kutuma vikosi vya polisi Haiti

Bunge la Kenya leo Alhamisi limeidhinisha kutumwa kwa maafisa wa polisi elfu moja katika nchi ya Haiti iliyotumbukia katika machafuko na ghasia za magenge yenye silaha.

Polisi hao wa Kenya ni sehemu ya ujumbe unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa unaotumwa Haiti kurejesha amani, licha ya ukosoaji mkubwa wa ndani. Hatua hii inakuja baada ya mahakama nchini Kenya kusitisha mpango huo kwa muda.

Uamuzi wa serikali ya Nairobi wa kutuma ujumbe wa polisi elfu moja huko Haiti umepingwa na baadhi ya wanasiasa wa Kenya wakiongozwa na kinara wa kambi ya upinzani, Raila Odinga, ambaye amesema kuwa mpango wa kutuma polisi nchini Haiti si kipaumbele cha Kenya.

Odinga alisisitiza kuwa ukanda wa Afrika Mashariki bado unakabiliwa na kile alichokitaja kama changamoto za kutosha.

 Waziri mkuu huyo wa zamani wa Kenya alisema hali ya Haiti ni hatari, akionya kwamba kutumwa polisi nchini humo kunahatarisha maisha ya polisi wa Kenya.

Wakati huo huo Dkt. Ekuru Aukot kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Party aliyewasilisha kesi ya kupinga kutumwa polisi wa Kwenya nchini Haiti amesema: "Bunge letu limeuza roho yake kwa Marekani na kwenda kusafisha fujo walizosababisha huko Haiti."

Ekuru Aukot

Vilevile raia wa Haiti wanaoishi nje ya nchi wameshutumu Kenya kwa kukubali kutuma polisi nchini mwao kudumisha amani na kupambana na magenge ya wahalifu nchini humo.

Raia wa Haiti walionekana wakiwa wamebeba mabango yenye maandishi ya kuilaani Kenya na kuitaja kama “kikaragosi cha Marekani”.

Mabango mengine yameandikwa maneno yanayomsawiri Rais William Ruto wa Kenya kama ‘kibaraka’ wa Marekani na kuitaka Washington iondoke nchini Haiti ikilaumiwa kwamba inayapa silaha magenge hayo.

Vilevile mashirika yasiyo ya kiserikali ya kutetea haki za binadamu yanaeleza kuwa polisi wa Kenya wamezoea kutumia mabavu, wakati mwingine ukatili mbaya dhidi ya raia, jambo ambalo ni hatari kubwa katika nchi ya Haiti ambako uingiliaji kati wa hapo awali wa kigeni umeandamana na ukiukaji wa haki za binadamu.

Tags