Wakazi wa Magharibi mwa Sudan Kusini wakimbia mapigano
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limeripoti kuwa wakazi wa eneo moja huko magharibi mwa Sudan Kusini wameyakimbia makazi yao kufuatia kujiri mapigano ya silaha kati ya jeshi la Sudan Kusini na makundi yenye silaha.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limetangaza kuwa watu elfu sabini wameyakimbia makazi yao kufuatia kujiri mapigano kati ya jeshi la Sudan Kusini na makundi yenye silaha katika eneo la Wau makao makuu ya mkoa wa Bahrul Ghazal magharibi mwa Sudan Kusini. Ripoti ya Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka imeongeza kuwa eneo la Wau limekumbwa na wimbi jipya la mapigano na machafuko tangu tarehe 26 mwezi Juni mwaka huu hadi sasa. Shirika hilo limesema kuwa mapigano kati ya jeshi la Sudan Kusini na makundi yenye silaha yamesababisha maelfu ya raia kuyaacha makazi yao na kuelekea katika maeneo ya kaskazini mwa Sudan Kusini. Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limetoa ripoti yake inayoonyesha kuwa maelfu ya raia katika jimbo la Bahrul Ghazal wamekimbilia kaskazini mwa jimbo la Darfur yaani Magharibi mwa Sudan; jimbo ambalo lenyewe linakabiliwa na uhaba wa maji na chakula.