Dec 08, 2023 14:28 UTC
  • Mahakama ya Zimbabwe yawazuia wabunge wa upinzani kushiriki uchaguzi muhimu wa kesho Jumamosi

Mahakama ya Zimbabwe imewazuia wagombea wengi wa upinzani kushiriki katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufnyika siku ya Jumamosi ya kesho ambao yumkini ukakiwezesha chama tawala cha ZANU-PF kufanya mabadiliko ya katiba.

Uamuzi huo ni mabadiliko ya hivi karibuni katika vita vya kukidhibiti chama cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC) huku kukiwa na mvutano mkubwa wa kisiasa katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

Mahakama ya Harare imeamuru kwamba wawakilishi 8 kati ya 9 wa chama kikuu cha upinzani, CCC, hawatagombea katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika kesho tarehe 9 Desemba na kwamba majina yao hayajajumuishwa kwenye upigaji kura.

Chama cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC) tayari kimekata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama uliotangazwa jana Alkhamisi, siku mbili kabla ya uchaguzi wa Jumamosi ya kesho. 

Msemaji wa chama cha CCC, Promise Mkwananzi amesema uamuzi huo unaonyesha "tabia ya kangaroo" ya mahakama za Zimbabwe na "kudorora kwa demokrasia" tangu Rais Emmerson Mnangagwa aingie madarakani mwaka 2017.

Ushindi wa chama tawala cha ZANU-PF katika uchaguzi mdogo wa kesho utakifanya kikaribie kupata theluthi mbili ya wingi wa kura za wabunge zinazohitajika kufanya marekebisho ya katiba.

Emmerson Mnangagwa

Wachambuzi wanaamini kuwa chama hicho kinataka kuondoa ukomo wa mihula miwili ya urais, na kumruhusu Rais Emmerson Mnangagwa, 81, kuimarisha udhibiti wake katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Tags