Mkuu wa upinzani DRC apuuza waranti ya kukamatwa dhidi yake
Moise Katumbi, kinara wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amepuuzilia mbali waranti ya kukamatwa iliyotolewa dhidi yake na serikali ya nchi hiyo na kusema kuwa atarejea nchini karibuni hivi kwa ajili ya kuwania urais.
Katumbi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, hatiwi wasiwasi na kile alichokitaja kuwa waranti 'bandia' ya polisi dhidi yake na kusisitiza kuwa hana hatia yeyote. Mwanasiasa huyo aliyetangaza nia ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi ujao na ambaye anakabiliwa na kesi ya kuajiri mamluki wa kigeni yuko bara Ulaya kwa ajili ya matibabu. Mgombea huyo wa muungano wa upinzani alikuwa amewasilisha ombi la kwenda kutibiwa nje ya nchi, ombi ambalo lilikubaliwa na serikali ya Kinshasa. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inadai kuwa, ina nyaraka na ushahidi unaoonesha kuwa, Meya huyo wa zamani wa Katanga alihusika katika kusajili mamluki wa kigeni wakiwemo askari kadhaa wa Kimarekani waliostaafu kwa lengo la kutekeleza njama dhidi ya taifa.
Wafuasi wake wanasema kuwa, tangu kiongozi wao atangaze nia yake hiyo ya kuwania kiti cha urais amekuwa akiandamwa na serikali ya Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001.