"Iran na Misri kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia karibuni"
Afisa wa ngazi za juu wa Misri amesema nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na Iran zinatazamiwa kufufua kikamilifu uhusiano wa pande mbili wa kidiplomasia, na hata kubadilishana mabalozi.
Rakha Ahmad Hassan, mwanachama wa Baraza la Masuala ya Kigeni la Misri amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik la lugha ya Kiarabu na kueleza kuwa, "Kubadilishana mabalozi ni suala ambalo yumkini litafanyika karibu hivi."
Amesema katika mustakabali wa karibu, uhusiano wa Iran na Misri utafufuliwa na kutashuhudia kufunguliwa balozi za pande mbili katika miji mikuu ya nchi hizo mbili hizi, Tehran na Cairo.
Afisa huyo mwandamizi wa Misri ameashiria mazungumzo ya simu ya karibuni baina ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na rais mwenzake wa Misri na kusema: Kiwango cha sasa cha mahusiano baina ya nchi mbili kinaashiria kuwa, suala la kubadilishana mabalozi lipo karibu. Aidha kauli ya karibuni ya kiongozi wa Oman, Sultan Haitham bin Tarik inaashiria kuwa jitihada zinaendelea katika eneo katika uwanja huo, kwa kuwa aligusia kuhusiana na kadhia hiyo na matokeo ya kuhuishwa mahusiano hayo.
Siku chache zilizopita, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifanya mazungumzo ya na rais mwenzake wa Misri, Abdel Fattah el Sisi na kutilia mkazo udharura wa kustawishwa uhusiano wa nchi hizi mbili katika nyuga tofauti.
Katika mazungumzo hayo, Sayyid Raisi mbali na kumpongeza Sisi kwa kushinda muhula mwingine wa urais, alisema, Iran na Misri zina historia ndefu ya uhusiano wa pamoja wa kiitikadi na kihistoria na hiyo ni fursa nzuri ya kuimarishwa uhusiano wa nchi hizi mbili katika nyuga zote.
Kwa upande wake, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri alipongeza siasa za Jamhuri ya Kiislamu za kuhakikisha inakuwa na uhusiano mzuri na nchi zake jirani na za ukanda huu mzima na kusema kuwa, kuna wajibu wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kuondoa vizuizi vyote vilivyopo ili kufufua uhusiano wa Misri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ikumbukwe kuwa, Misri ilikata uhusiano wake na Iran mwaka 1980 baada ya nchi hiyo ya Kiarabu kumpokea mtawala aliyepinduliwa wa Iran, Mohammed Reza Pahlavi; mbali na Cairo kuutambua utawala wa kibaguzi wa Israel.