Jan 27, 2024 07:29 UTC
  • Uganda yajitenga na jaji wa ICJ aliyepiga kura kwa maslahi ya Israel

Uganda imejiweka mbali na hatua ya Julia Sebutinde, jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) raia wa nchi hiyo, ya kupiga kura kupinga vipengee vya maagizo yaliyotolewa na mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni Israel kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo pandikizi katika Ukanda wa Gaza dhidi ya Wapalestina.

Adonia Ayebare, Mwakilishi wa Kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa amesema katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: Uamuzi wa Jaji Sebutinde katika ICJ hauakisi msimamo wa serikali ya Uganda kuhusu hali ya Palestina.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Uganda amesisitiza kuwa, Kampala inaliunga mkono taifa la Palestina, na hili linadhihirika wazi kwa namna mara zote nchi hiyo ya Afrika Mashariki inavyopiga kura kwa maslahi ya Palestina katika Umoja wa Mataifa.

Jaji huyo wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) raia wa Uganda ameshambuliwa vikali na watu wa matabaka mbalimbali wakiwemo watuamiaji wa mitandao ya kijamii hasa wa Afrika Mashariki kwa uamuzi wake huo wa kuikingia kifua Israel.

Mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Gaza

Mmoja wa watumiaji wa mtandao wa kijamii wa X raia wa Kenya ameandika: Jaji Julia Sebutinde ni fedheha kwa nchi yake na kwa ubinadamu. Hakupiga kura tu dhidi ya shauri la Afrika Kusini, bali dhidi ya mantiki, maadili, haki, uhuru na upendo. Amepiga kura dhidi ya roho ya ubinadamu.

Sebutinde alikuwa jaji pekee wa ICJ aliyepiga kura kupinga maamuzi ya dharura ya mahakama hiyo ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendelea kuua watoto na wanawake wa Palestina Gaza.

 

Tags