Apr 07, 2024 07:02 UTC
  • Kenya yajipanga kununua silaha mpya za kisasa za kivita kukabiliana na ongezeko la uhalifu

Serikali ya Kenya imetangaza kuwa imo mbioni kununua silaha mpya za kisasa za kivita ili kukabiliana na ongezeko la uhalifu nchini humo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, alizindua silaha za kisasa zenye thamani ya shilingi bilioni 7.6 kukabiliana na utovu wa usalama nchini humo.

Tayari Rais wa nchi hiyo William Ruto ameahidi kuwa ununuzi wa silaha hizo ni mwanzo tu wa mchakato wa serikali kununua zana za kisasa za kivita kukabiliana na uhalifu.

Rais William Ruto

Wiki iliyopita, Ruto aliongoza mkutano wa maafisa wa ngazi za juu wa usalama, ambapo aliahidi kuwa, serikali itatoa ndege zaidi kwa Idara ya Polisi kuisaidia kukabilana na uhalifu.

Wizara ya Usalama wa Ndani imeagizwa kuharakisha mchakato wa kuwapa polisi silaha hizo.

Serikali ya Kenya imetangaza kwamba, kwa miaka mitatu ijayo, itatenga jumla ya shilingi bilioni 29.4 kuendesha Mpango wa Kuwapa Polisi Silaha za Kisasa (PEM).

Mpango huo unalenga kuhakikisha Polisi wamepata sare, magari yaliyojizatiti, magari ya kuhimili miripuko, droni, helikopta za kuwakabili wahalifu, mashine za kuondoa mada za miripuko na kadhalika.../

 

Tags