Apr 01, 2024 10:40 UTC
  • Seneti ya Kenya: Watuhuniwa wa mbolea feki wafunguliwe mashtaka

Maseneta wa Kenya wametaka maafisa wa serikali walioruhusu mbolea feki kuingia nchini humo na katika mabohari ya Bodi la Nafaka na Mazao (NCPB) wafikishwe mahakamani.

Ni baada ya Baraza la Seneti ya Kenya kuwaagiza mawaziri Mithika Linturi (Kilimo), Rebecca Miano (Biashara) na maafisa wa Halmashauri ya Kukagua Ubora wa Bidhaa Kenya (Kebs), kufika mbele yake ili kuhojiwa, kuhusiana na uuzaji na usambazaji wa mbolea feki nchini humo.

Maseneta hao vilevile wanataka maafisa husika, wakipatikana na hatia, wawarejeshee pesa wakulima walionunua mbolea hiyo.

Kutokana na sakata hiyo, mamia ya wakulima wamelalamika kupoteza maelfu ya pesa baada ya kuuziwa mbolea feki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo, James Murango, amesema wameanzisha uchunguzi kuhusu jinsi mbolea hiyo feki ilivyoingia nchini huku wakimulika Shirika linalosimamia Viwango vya Ubora Nchini (Kebs) na Shirika la Kitaifa la Biashara (KNTC).

“Kilio cha mbolea feki kimetufikia. Kama Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo, tunataka kuchunguza ili tujue ikiwa kuna hujuma. Iwapo ni hujuma, basi mbolea hiyo ilifikaje katika mabohari ya NCPB? Tunataka kujua ni vipi Kebs haikuwa na habari kwamba mbolea ghushi ilikuwa inasambazwa kwa wakulima,” amesema Bw Murango.

Seneta huyo amehoji kwamba, swali kuu ni juu ya jinsi mbolea hiyo iliweza kupenya katika mabohari ya NCPB yanayomilikiwa na serikali bila kugunduliwa.

Seneta Murango amesema: "Inasikitisha kwamba wakulima wengi wanagundua tatizo hilo baada ya kununua mbolea. Wanafungua mifuko na kupata mchanga, kinyesi cha punda na mawe."

Tags