Jul 11, 2016 07:49 UTC
  • Al-shabaab washambulia kambi ya jeshi na kuua askari 10

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limeshambulia kwa bomu kambi moja ya jeshi kusini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia Mogadishu na kuua wanajeshi 10 wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Ahmed Farah, ofisa wa jeshi la Somalia katika mji unaopakana na Mogadishu wa Afgooye ameliambia shirika la habari Reuters kuwa, gaidi mmoja wa al-Shabaab aliingia na gari lililokuwa na mabomu ndani ya kambi hiyo na kisha sauti kubwa ya mripuko ikasikika mapema leo. Wakati huohuo, kundi hilo la wakufurishaji limekiri kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi na kusema kuwa, idadi ya askari wa jeshi la Somalia waliouawa katika shambulizi hilo ni 30.

Haya yanajiri siku chache baada ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kutangaza kuwa askari wa umoja huo wanaohudumu huko Somalia chini ya mwavuli wa kikosi cha AMISOM watendelea kusalia nchini humo hadi Disemba mwaka 2020. Kundi la kitakfiri la al-Shabaab limekuwa likitekeleza mashambulizi ya kigaidi ndani na nje ya Somalia.

Tags