Uchunguzi wa maoni: Uungaji mkono kwa ANC Afrika Kusini unazidi kupungua
(last modified Thu, 11 Apr 2024 07:54:21 GMT )
Apr 11, 2024 07:54 UTC
  • Uchunguzi wa maoni: Uungaji mkono kwa ANC Afrika Kusini unazidi kupungua

Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa nchini Afrika Kusini umekuwa na habari mbaya zaidi kwa Rais Cyril Ramaphosa na chama chake tawala cha African National Congress (ANC) baada ya kuonyesha kuwa uungaji mkono kwa chama hicho unazidi kupungua.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Wakfu wa Utafiti wa Kijamii, umeonyesha kuwa chama hicho kinaweza kupata asilimia 37 ya kura katika uchaguzi wa tarehe 29 Mei.
 
Pia umegundua kuwa chama kipya kilichodunishwa cha Rais wa zamani Jacob Zuma cha Umkhonto weSizwe (MK), kinaweza kuwa cha tatu kwa ukubwa nchini humo baada ya uchaguzi wa mwezi ujao.
 
Siku ya Jumanne, Mahakama ya Uchaguzi ilitoa uamuzi kwamba Zuma anaweza kugombea katika uchaguzi licha ya kifungu cha Katiba kinachozuia wagombea ambao wamewahi kutumikia kifungo cha miezi 12 au zaidi.
Jacob Zuma

Katika uchaguzi wa 2019, ANC ilipata asilimia 57,5 ya kura, chini yake tangu kuchukua madaraka mwaka 1994.

 
Matokeo ya chini ya asilimia 50 ya kura kiliyotabiriwa kupata ANC yanamaanisha kuwa kitalazimika kuingia katika muungano na vyama vidogo ili kuweza kuongoza tena nchi.
 
Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa hivi karibuni na taasisi ya Brenthurst Foundation na SABI Strategy Group ulikadiria uungwaji mkono wa ANC kuwa umefikia asilimia 39.
 
Hata hivyo chama cha tatu kwa ukubwa nchini Afrika Kusini bungeni, EFF kiliyatilia shaka matokeo ya uchunguzi huo.
 
Umaarufu wa ANC umekuwa ukipungua kutokana na kuwepo mdororo wa kiuchumi, ukosefu mkubwa wa ajira, kashfa za ufisadi, kukatika kwa umeme na kukitihiri uhalifu nchini Afrika Kusini.../