Apr 13, 2024 02:45 UTC
  • Tume ya Uchaguzi Afrika Kusini yaitaka mahakama ya juu kutatua suala la kugombea kwa Zuma

Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini imesema kuwa imekata rufaa katika Mahakama ya Juu zaidi nchini humo ikiiomba kutoa uamuzi kuhusu iwapo rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma, anaweza kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu mwezi Mei au la.

Tume hiyo ilisema katika taarifa yake jana Ijumaa kwamba imewasilisha rufaa "ya dharura na ya moja kwa moja" kwa Mahakama ya Kikatiba ili kutoa "uhakika" juu ya tafsiri sahihi ya kifungu cha katiba kinachohusiana na kugombea kwa watu ambao wamepatikana na hatia.

"Uwazi kama huo ni muhimu katika suala la sasa lakini pia kwa chaguzi zijazo," imesema taarifa hiyo.

Rufaa hiyo ni hatua ya karibuni zaidi katika mzozo wa kisheria unaohusu ustahiki wa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 81, kugombea katika uchaguzii ujao, baada ya mahakama ya uchaguzi kuamua wiki hii kuwa Zuma anaweza kuwania nafasi hiyo, na kubatilisha uamuzi wa awali uliokuwa umemzuia kugombea.

Zuma anatarajia kugombea urais kwa tiketi ya chama cha Umkhonto weSizwe Party (MK), ambacho alijiunga nacho mwaka jana baada ya kukitupia madongo chama tawala cha African National Congress (ANC) ambacho aliwahi kukiongoza.

Tarehe 29 Mei, raia wa Afrika Kusini watapiga kura kuwachagua wajumbe 400 wa Bunge. Mwezi mmoja baadaye, wabunge katika bunge jipya watachagua rais ajaye.

Kwa kuzingatia umaarufu wa Zuma, chama cha MK kinatarajia kushinda kura za kutosha ambazo zitakihakikishia viti vya bunge, na kumega sehemu ya kura za chama cha ANC.

Ripoti zinasema, kuna uwezekano idadi ya viti vya ANC ikashuka chini ya asilimia 50 kwa mara ya kwanza tangu 1994.

Wachambuzi wanasema, upungufu wa wabunge, utailazimisha ANC kutafuta washirika ili kusalia madarakani, suala ambalo litamfanya Zuma kuwa turufu muhimu katika kinyang'anyiro cha kumchagua raia ajaye wa Afrika Kusini. 

Tags