Apr 14, 2024 11:10 UTC
  • Waniger waandamana kutaka majeshi ya kigeni yaondoke nchini mwao

Mamia ya watu wameshiriki katika maandamano ya kupinga uwepo wa majeshi ya kigeni nchini Niger, vikiwemo vikosi vya jeshi vya Marekani ambayo ina kambi ya kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo.

Waandamanaji hao wamekusanyika katikati mwa mji mkuu wa Niamey, kuitikia wito wa mashirika ya kiraia yaliyo karibu na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo ambao baadhi ya maafisa wake wameshiriki pia katika maandamano hayo.
 
Abdoulaziz Yaya, mmoja wa waandamanaji amesema: "tumetoa wito wa kuondoka Wamarekani na vikosi vyote vya kigeni kutoka Niger, na uongozi wa jeshi umezingatia wasiwasi wetu, na ni katika muktadha huu kwamba tumekuja kuunga mkono na kuthibitisha uungaji mkono wetu kwa uongozi wa jeshi kuhusiana na uamuzi uliochukuliwa wa kutaka majeshi ya kigeni yaondoke".
 
Maandamano hayo yamefanyika wakati taifa hilo la Afrika Magharibi likijiondoa katika ushirikiano wa karibu na Marekani katika juhudi za kukabiliana na ugaidi, na badala yake kuigeukia Russia kwa ajili ya masuala yake usalama.

Maandamano hayo yanaonekana kama hatua zaidi ya kuitaka Washington ijiondoe nchini Niger baada ya wanajeshi wa Russia kuwasili nchini humo wiki iliyopita kwa ajili ya kudhamini usalama wa serikali ya kijeshi inayotawala.

 
Kuhusiana na hilo mmoja wa walioandaa maandamano hayo, Moumouni Amadou Gado amesema: "Warussia watakuwa hapa kama sehemu ya ushirikiano wa manufaa ya pande mbili, wakati Wamarekani, kama tulivyoona, wamekuwa hapa kwa miaka ngapi? Je, ukosefu wa usalama umepungua? Nitasema hapana. Lakini kwa upande wa Warussia hivi majuzi tumeona hali inaboreka".
 
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, Baraza tawala la kijeshi la Niger, linalojulikana kama CNSP, bado halijawaamuru wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini humo.
 
Hata hivyo kwa kuwasili vikosi vya Russia, itawawiya vigumu wanajeshi wa Marekani pamoja na wafanyakazi wa kidiplomasia na wa kiraia kuendelea kubaki nchini Niger.../

Tags