Apr 24, 2024 12:23 UTC
  • Wachambuzi: RSF huenda ikaunda serikali katika eneo la Darfur

Waangalizi wa mambo wanahofia kuwa eneo la Darfur magharibi mwa Sudan litaingia kwenye machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya gavana wa eneo hilo na mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Sudan, Minni Arko Minawi, kuwatuhumu wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kuwa wanapanga kuunda serikali katika eneo hilo baada ya kabila la Zaghawa kutangaza kujiunga na jeshi la Sudan dhidi ya RSF.

Minawi ameituhumu RSF kuwa inapanga kuunda serikali mpya magharibi mwa Sudan ambayo amesema "itatambuliwa kimyakimya."

Katika muktadha huo, mtafiti aliyebobea katika masuala ya Darfur, Ali Mansour Hasballah, anasema kwamba taarifa zinazosambazwa katika duru zilizo karibu na RSF zinaonyesha kwamba kundi hilo linaelekea kuitenga Darfur ili kutangaza serikali katika eneo hilo, baada ya kushindwa kunyakua madaraka huko Khartoum na kudhibiti nchi.

Hasballah amesema, Kamandi ya RSF iliamua kudhibiti El Fasher kwa msaada wa vyama vya kikanda, baadhi ya makundi katika nchi jirani za eneo hilo na kwa kutumia mamluki na makundi yenye silaha huko Darfur.

Siku chache ziliizopita Minni Arko Minawi, mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Sudan (SLM) ambaye pia ni gavana wa jimbo la Darfur, alitangaza kuwa vikosi vya harakati hiyo vinaelekea katika mji mkuu, Khartoum, kushirikiana na jeshi la taifa katika mapambano dhidi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Tangu katikati ya Aprili 2023, jeshi la Sudan likiongozwa na mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala, Abdel Fattah al-Burhan, limekuwa katika vita vikali na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vinavyoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo, na hadi sasa mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 13,000 na takriban milioni 8.5 wamelazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya Sudan.