Apr 28, 2024 04:27 UTC
  • Afrika Kusini yaadhimisha miaka 30 ya uhuru

Afrika Kusini imeadhimisha miaka 30 ya uhuru na demokrasia baada ya kumalizika utawala wa kandamizi na wa kibaguzi, ikiwa ni takribani mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi nchini humo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Akihutubia hapo jana katika maadhimisho hayo, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alipongeza mafanikio ya nchi hiyo chini ya uongozi wa chama chake cha African National Congress (ANC).

"Afrika Kusini leo ipo mahali pazuri zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 30 iliyopita," Ramaphosa alisema katika hotuba yake ya kuadhimisha "Siku ya Uhuru" katika Majengo ya Muungano mjini Pretoria ambayo ndio makao makuu ya serikali.

Ramaphosa alitumia maadhimisho hayo kuelezea mafanikio na maboresho yaliyofanywa na chama cha ANC, ambacho kinakabiliwa na ushindani mkali katika uchaguzi ujao huku kikiwa katika hatari ya kupoteza kwa mara ya kwanza wingi wa wabunge.

Ramaphosa amesema: "Tumefuatilia mageuzi ya ardhi, na kutoa mamilioni ya hekta za ardhi kwa wale waliopokonywa ardhi zao kwa nguvu, tumejenga nyumba, zahanati, hospitali, barabara na kujenga madaraja, mabwawa, na miundombinu kadhaa. Tumesambaza umeme na maji safi kwa mamilioni ya kaya za Afrika Kusini.

 

Wananchi wa Afrika Kusini watapiga kura tarehe 29 ya mwezi ujao wa Mei miongo mitatu baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1994 uliotamatisha utawala kandamizi wa wazungu, na kumuweka madarakani Nelson Mandela na chama chake cha ANC.

Kura ya maoni iliyofanywa na shirika la Ipsos na iliyotolewa siku ya Ijumaa imeonyesha kuwa uungwaji mkono kwa chama tawala ANC, ambacho kilipata zaidi ya asilimia 57 ya kura katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2019, umeshuka hadi zaidi ya asilimia 40.    

Iwapo ANC itapa ushindi ulio chini ya asilimia 50, basi chama hicho kitalazimika kutafuta washirika wa kuunda serikali ya mseto ili kusalia madarakani.