May 26, 2024 07:07 UTC
  • Burkina Faso yarefusha muda wa utawala wa kijeshi kwa miaka mitano baada ya mashauriano ya kitaifa

Kanali Moussa Diallo Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mchakato wa mazungumzo ya kitaifa ya Burkina Faso amesema kuwa wameainisha muda wa kipindi cha mpito kuwa miezi 60 kuanzia Julai Pili mwaka huu.

Ameongeza kuwa, kiongozi wa mapinduzi na Kaimu Rais Ibrahim Traore wanaweza kugombea urais katika uchaguzi wowote baada ya kumalizika kipindi cha mpito. Jeshi limekuwa madarakani huko Burkina Faso tangu mwaka 2022 kwa kufanya mapinduzi mawili  ambayo yamehalalishwa katika maeneo mengi ya nchi hiyo kutokana na ukosefu wa usalama nchini humo. 

Makundi yenye silaha yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na kundi la Daesh (ISIS) yamekuwa yakitekeleza mashambulizi na kuibua hali ya mchafukoge nchini Burkina Faso tangu mwaka 2015; hujuma ambazo zimepelekea kuuliwa maelfu ya watu na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. 

Mazungumzo ya awali ya kitaifa ya Burkina Faso yalipasisha makubaliano ambayo yalimteuwa Traore kuwa Rais na kuainisha serikali na bunge. Makubaliano hayo yaliainisha kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia ambacho muda wake unamalizika Julai Mosi mwaka huu, hata hivyo  Rais wa mpito Ibrahim Traore ametahadharisha mara kadhaa kwamba itakuwa vigumu kuendesha uchaguzi huko Burkina Faso kutokana na hali mbaya ya usalama. 

Ibrahim Traore 

 

Tags