Jun 14, 2024 04:06 UTC
  • Bajeti Afrika Mashariki: Wastaafu watabasamu Tanzania, Uganda kupambana na deni la taifa

Mawaziri wa fedha wa Afrika Mashariki wamewasilisha mipango yao ya matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 huku pakiwa na mazingira magumu ya kiuchumi na kero kubwa la kupanda kwa madeni ya umma.

Kero zingine ni gharama ya juu ya mafuta, kushuka kwa mapato,hali ngumu ya biashara na mivutano ya kimataifa ya kijiografia katika Mashariki ya Kati na Ulaya Mashariki mambo ambayo yanachangia kuzuia ukuaji wa uchumi katika ukanda huo.

Waziri wa Fedha nchini Kenya Prof. Njuguna Ndung'u Alkhamisi aliwasilisha mapendekezo ya bajeti ya sh3.9 trilioni huku akiiyapa kipaumbele maeneo makuu matano yakiwemo ya kilimo, huduma za afya, nyumba na makazi na Uboreshaji wa miundo ya Kidijitali na tasnia ya ubunifu.

Nchini Tanzania Waziri wa fedha Mwigulu Nchemba amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/2025 ambayo ni shilingi trilioni 49.3 sawa na ongezeko la asilimia 11.2 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita.

 

Miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa gumzo kubwa katika siku za karibuni ni malipo ya pensheni kwa wastaafu ambapo sasa Serikali imeongeza malipo ya mkupuo kwa asilimia 7 kutoka asilimia 33 ya sasa hadi asilimia 40.

Uganda inatarajia kupunguza deni linaloongezeka kwa kuzingatia ukopaji wa masharti nafuu na kuzuia mikopo ya kibiashara mwaka ujao wa fedha, waziri wake wa fedha Matia Kasaija alisema Alkhamisi, baada ya kushuka kwa kiwango cha mikopo mwezi uliopita.

Deni la umma la nchi hiyo ya Afrika Mashariki limekuwa likiongezeka huku serikali ya Rais Yoweri Museveni ikisitisha miradi mikubwa ya miundombinu, jambo ambalo limezusha onyo kutoka kwa benki yake kuu.

Tags