Jun 19, 2024 11:01 UTC
  • Moto wateketeza hifadhi ya silaha Chad, 55 wauawa na kujeruhiwa

Makumi ya watu wamefariki dunia huku wengine wengi wakijeruhiwa kutokana na ajali ya moto iliyoikumba hifadhi ya silaha na zana za kijeshi nchini Chad.

Waziri wa Afya wa Chad, Abdelmadjid Abderahim amewaambia waandishi wa habari leo Jumatano kuwa, kwa akali watu tisa wamethbitishwa kupoteza maisha kwenye mkasa huo wa moto wa jana usiku.

Ameongeza kuwa, watu karibu 50 wamejeruhiwa vibaya kwenye mkasa huo uliotokea katika kituo cha kuhifadhi silaha na zana za kijeshi kilichoko katika eneo la Goudji, viungani mwa mji mkuu, N’Djamena. 

"Tuna wasi wasi kwamba idadi ya walioaga dunia kwenye mkasa huo itaongezeka kutokana na hali mbaya ya majeruhi," ameongeza Waziri wa Afya wa Chad.

Rais Mahamat Idriss Deby Itno wa Chad

Rais Mahamat Idriss Deby Itno wa Chad sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye ajali hiyo, lakini pia amewatakia afueni ya haraka majeruhi.

Amesema katika taarifa kuwa, uchunguzi wa kubaini kiini na wahusika wa moto huo umeanzishwa. Aidha amewataka wananchi wa Chad kuwa watulivu huku vyombo vya dola vikiendelea kufanya uchunguzi.

Mashuhuda wamenukuliwa na shirika la habari la Anadolu wakisema kuwa, miripuko hiyo iliyosababishwa na moto kiwandani hapo ilisikika usiku kucha karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa N’Djamena. 

Tags