Ruto achukua hatua za kubana matumizi kufuatia maandamano ya vijana
Katika hatua za kubana matumizi, Rais William Ruto wa Kenya ametangaza kwamba atapunguza idadi ya washauri wa serikali kwa asilimia 50, huku watumishi wa umma waliofikisha umri wa kustaafu (miaka 60) wakitakiwa kuondoka kazini mara moja.
Rais Ruto alitangaza maamuzi hayo jana Ijumaa katika hotuba yake kwa taifa, kufuatia malalamiko na maandamano ya umma yakiongozwa na vijana wa kizazi cha sasa (Gen Z). Maandamano hayo yalimlazimisha Ruto kuuweka kando Mswada wa Fedha wa 2024 uliokuwa umejumuisha nyongeza ya kodi.
Kando na kupunguza idadi ya washauri, Rais Ruto alitangaza mpango wa kufuta mashirika 47 ya serikali ambayo yana kazi zinazofanana. Alisema watumishi kutoka katika mashirika hayo watapatiwa kazi nyingine katika wizara na idara mbalimbali ndani ya serikali.
Dakta Ruto amesema hatua hizo zinalenga kuondoa gharama, kurahisisha utendakazi wa serikali, na kuimarisha uratibu ndani ya utumishi wa umma.

Hata hivyo Ruto amepuuzilia mbali wito wa vijana wa kulivunja baraza zima la mawaziri na kuteua jipya. Akizungumza moja kwa moja na vijana kwenye mtandao wa kijamii wa X kupitia jukwaa la Space jana Ijumaa, Rais Ruto alisema atatumia njia nyingine za kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na wananchi dhidi ya baadhi ya mawaziri wake.
“Sitalivunja Baraza la Mawaziri kwa sababu niko katika harakati za kuangalia mambo kwa njia tofauti,” Rais Ruto alisema. Hata hivyo, Dakta Ruto aliwaonya mawaziri dhidi ya kujihusisha na shughuli za ufisadi na kusema kuwa yuko tayari kumfuta kazi waziri yeyote. Miongoni mwa matakwa ya vijana walioandamana ni mawaziri wanaohusishwa na ufisadi wafutwe kazi.