FAO yatahadharisha kuhusu mgogoro wa kibinadamu Sudan Kusini
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limetahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea mgogoro wa kibinadamu huko Sudan Kusini.
Shirika la FAO limesema kuwa mgogoro wa kibinadamu unaweza kushuhudiwa huko Sudan Kusini kutokana na baa la njaa iwapo machafuko yataendelea nchini humo.
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani limeashiria namna mamilioni ya watu huko Sudan Kusini wanavyotaabika kwa njaa na kuongeza kuwa, raia wa nchi hiyo watadhurika zaidi iwapo mapigano hayatasimamishwa haraka iwezekanavyo.
Shirika hilo limeashiria pia uhaba wa chakula nchini Sudan Kusini na kutaka kutumwa misaada ya kibinadamu nchini humo.
Wiki iliyopita pia Eugene Owusu, Mratibu wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini alieleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya katika maeneo yaliyoathiriwa na vita nchini humo.
Maelfu ya watu wamelazimika kuhama makazi yao na mamia ya wengine wameuawa kufuatia kujiri mapigano kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini.