Jul 17, 2016 15:54 UTC
  • Serikali: Vikwazo vimesababisha mgogoro wa kiuchumi Zimbabwe

Serikali ya Zimbabwe imelaumu vikwazo vya kimataifa na kusema kuwa ndiyo sababu kuu ya mgogoro wa kiuchumi unaoshuhudiwa nchini humo hivi sasa.

Patrick Chinamasa, Waziri wa Fedha wa Zimbabwe amesema, vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo na nchi za Magharibi tangu mwaka 2001 ndivyo vimepelekea kuzuka mgogoro mkubwa wa kiuchumi nchini humo, uliopelekea watumishi wa umma wakiwemo wanajeshi wa nchi hiyo kucheleweshewa mishahara yao. Chinamasa ameliambia shirika la habari la Reuters mjini Kigali, pambizoni mwa kongamano la Umoja wa Afrika kuwa, vikwazo hivyo vimesababisha serikali ya Harare kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kimataifa kama kulipa madeni, jambo ambalo limelifanya Shirika la Fedha Duniani IMF kukataa kuipa nchi hiyo mkopo tangu mwaka 1999. Zimbabwe inadaiwa na IMF dola bilioni 1.8 za Kimarekani. Ijumaa iliyopita, ilibainika kuwa, Zimbabwe imeshindwa kulipa kwa wakati mishahara ya jeshi la nchi hiyo kwa mwezi wa pili mfululizo sasa.

Ucheleweshaji huo wa mishahara ya jeshi la Zimbabwe unatazamia kuchochea mivutano nchini humo ambayo tayari imekumbwa na ukame, kushuka kwa bei za madini na uhaba mkubwa wa fedha; masuala ambayo yote yamesababisha maandamano mwezi huu nchini humo dhidi ya Rais Robert Mugabe.

Tags