Sep 09, 2024 13:06 UTC
  • Takwa la Umoja wa Mataifa la kuwekewa vikwazo Israel

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya chakula amesema kuwa, Israel sio tu inazuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza, bali pia inaharibu ardhi na vyanzo vya chakula vya Palestina.

Hapo awali pia Michael Fakhri alitangaza katika ripoti yake kwamba, Desemba 2023, wakaazi wa Ukanda wa Gaza walikuwa wakiunda 80% ya watu waliokumbwa na njaa ulimwenguni, na hakuna rekodi katika historia ya vita inayoonyesha kwamba, kuna taifa lilikumbwa na njaa kwa kasi ya kiwango hiki. Nukta muhimu ni kwamba hali ya wakazi wa Gaza kutokana na kuendelea vita vya kikatili vya utawala wa Kizayuni dhidi yao kwa upande mmoja na kuzuiwa kutumwa misaada ya kimataifa ya kibinadamu kwa upande wa pili kunakofanywa na Israel, hivi sasa ni mbaya zaidi na ya kutisha kuliko hapo kabla.

Hii si mara ya kwanza kwa taasisi za kimataifa na kieneo kutoa mwito wa kuwekewa vikwazo Israel kutokana na jinai zake ambazo hazijawahi kushuhudiwa katika vita vya Gaza. Mwishoni mwa Agosti 2024, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Euro-Mediterranean lilionya katika taarifa yake kuhusu amri za mara kwa mara za utawala wa Kizayuni za kuwataka Wapalestina huko Gaza wahame na kuzitaka nchi za dunia ziuwekee vikwazo utawala huo ghasibu na wakati huo huo zisitishe himaya na uungaji mkono wao kwa utawala huo.

 

Suala hili linapata maana zaidi hasa kwa kuzingatia ongezeko la idadi ya kutisha ya mashahidi na Wapalestina na waliojeruhiwa wanaoishi Gaza kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni, ambayo yamezusha maandamano makubwa duniani zikiwemo nchi za Ulaya na Marekani. Kulingana na takwimu, idadi ya mashahidi ambao wengi wao ni watoto na wanawake imefikia 41,000 na idadi ya waliojeruhiwa imepindukia 95,000, na sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza imeharibiwa kabisa.

Katika vita hivyo, mbali na kuenea kwa uharibifu na njaa iliyochukua maisha ya mamia ya watoto wa Kipalestina na kuhesabiwa kuwa ni miongoni mwa majanga mabaya zaidi ya binadamu duniani, zaidi ya Wapalestina 10,000 wametoweka pia na hadi sasa hawajulikani walipo.

Bila shaka jinai hizi za kutisha zisingewezekana bila msaada mkubwa wa kijeshi na silaha wa Marekani, ambayo imeupelekea takriban tani 50,000 za silaha na risasi utawala ghasibu wa Israel. Licha ya kwamba kumekuwepo na maandamano makubwa ya wananchi hasa wanafunzi na wasomi ndani ya Marekani kwa ajili ya kupinga na kulalamikia sera ya serikali ya Biden kuhusiana na Israel, lakini Ikulu ya White imeendelea na mchakato wa kuupa silaha utawala wa Kizayuni wa Israel.

Aidha, nchi nyingine za magharibi pia zimedumisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na hata kijeshi na Tel Aviv, licha ya hatua hiyo kulaaniwa waziwazi, na hivyo kuusaidia utawala wa Kizayuni katika kuendeleza na vitendo vyake vya jinai. Bila shaka, majaribio mengi yamefanywa barani Ulaya na Marekani ya kuuwekea vikwazo vya silaha utawala wa Kizayuni. Kwa mfano, Mei 2024, wawakilishi 88 wa chama cha Demokrasia katika Bunge la Marekani, katika barua kwa Rais wa Marekani Joe Biden, walitaka kupigwa marufuku uuzaji wa silaha kwa Israel.

Barani Ulaya, mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu yameomba kuacha kupelekwa zana za kijeshi na silaha kwa Israel.

Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa kampeni kubwa katika maeneo mbalimbali ya dunia ya kuutenga na kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel na hata kususia bidhaa zinazotengenezwa na utawala huo bandia.

 

Suala muhimu ni kwamba, licha ya kulaaniwa na kuenea kimataifa vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Gaza, lakini hakuna hatua zozote za kimataifa zilizoratibiwa za kuuwekea vikwazo utawala huo na tumeshuhudia tu hatua za mtu binafsi za baadhi ya nchi. Katika suala hili, Rais wa Colombia, Gustavo Petro, alitangaza mnamo Agosti 21, 2024 kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba nchi hiyo imeacha rasmi kusafirisha makaa ya mawe kwa Israel.

Aidha Colombia ilikata uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni miezi miwili iliyopita. Hatua hii, ambayo inaweza kuchukuliwa kama utangulizi wa hatua kama hizo kwa nchi nyingine, imekaribishwa na Hamas. Katika taarifa yake Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS sambamba na  kukaribisha hatua ya serikali ya Colombia imesisitiza kuwa, nchi nyingine za dunia nazo zinapaswa kuiga mfano huo na kususia na kuitenga serikali ya kibaguzi ya Israel ambayo inafanya mauaji ya kimbari huko Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza kwa himaya na uungaji mkono wa Marekani na washirika wake.

Tags