UNHCR: 70% ya wakimbizi wa Sudan Kusini ni watoto
Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi wa la Umoja wa Mataifa limeeleza wasiwasi wake juu ya ongezeko la wakimbizi wa Sudan Kusini na uhaba wa fedha za kuwahudumia wakimbizi hao; na kufichua kuwa asilimia 70 ya wakimbizi hao ni watoto wadogo.
Ann Encontre, Mratibu wa UNHCR nchini Sudan Kusini amesema, kati ya dola milioni 638 zilizoahidiwa na wafadhili kwa ajili ya wakimbizi wa nchi hiyo mwaka huu, asilimia 17 tu ya fedha hizo ndizo zimetolewa kufikia sasa na hivyo kuliweka shirika hilo katika hali ngumu. Amesema asilimia 23 ya fedha zinazohitajika, ni kwa ajili ya chakula na kusisitiza kuwa, Wasudan Kusini milioni 4.8 wanatazamiwa kukabiliwa na baa la njaa katika miezi michache ijayo. Mratibu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi wa la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ameongeza kuwa, kutokana na mapigano mapya kuzuka katika mji mkuu Juba hivi karibuni, idadi ya wakimbizi wa nchi hiyo inatazamiwa kupindukia milioni moja kabla ya kumalizika mwaka huu.
Kauli ya UNHCR inajiri muda mfupi baada ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO kutahadharisha kuwa, mgogoro wa kibinadamu unaweza kutokea huko Sudan Kusini kutokana na baa la njaa iwapo machafuko yataendelea.
Shirika la FAO limeashiria namna mamilioni ya watu wa Sudan Kusini wanavyotaabika kwa njaa na kuongeza kuwa, raia wa nchi hiyo watadhurika zaidi iwapo mapigano hayatasimamishwa haraka iwezekanavyo.