WHO yazindua mpango wa miezi sita wa kuzuia usambaaji wa Mpox
(last modified Tue, 27 Aug 2024 06:57:18 GMT )
Aug 27, 2024 06:57 UTC
  • WHO yazindua mpango wa miezi sita wa kuzuia usambaaji wa Mpox

Shirika la Afya Duniani WHO limezindua mpango wa miezi sita wa kusaidia kukomesha usambaaji wa maambukizi ya ugonjwa wa mpox.

Mpango huo unalenga pamoja na mambo mengine kuongeza wafanyakazi katika nchi zilizoathiriwa na mikakati ya ufuatiliaji, kinga na matokeo ya hatua zilizochukuliwa.
 
WHO imesema inatarajia mpango huo uataanza mwezi Septemba hadi Februari mwaka ujao na utahitaji ufadhili wa dola milioni 135 ukilenga kuboresha ufikiaji stahiki wa chanjo, hasa katika nchi za Kiafrika zilizoathiriwa zaidi na mripuko huo.
 
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameeleza katika taarifa aliyotoa: "miripuko ya mpox katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi jirani inaweza kudhibitiwa, na inaweza kukomeshwa,"
Ugonjwa wa Mpox

Siku ya Jumanne iliyopita, Kongo DR ambayo ndiyo nchi iliyoathiriwa zaidi na Mpox iliripoti zaidi ya kesi 1,000 mpya za ugonjwa huo katika wiki ya kabla yake.

 
Katika taarifa yake ya hivi punde kuhusu mripuko huo, Vituo vya Afrika vya Kudhibiti Magonjwa vimeripoti kuwa hadi kufikia Alkhamisi iliyopita, zaidi ya kesi 21,300 zinazoshukiwa au kuthibitishwa na vifo 590 vimeripotiwa katika nchi 12 za Afrika.
 
Mpoks unatokana na virusi kama vya ndui lakini kwa kawaida husababisha dalili zisizo kali kama vile homa, baridi na maumivu ya mwili. Huenea zaidi kwa mgusano wa karibu wa ngozi kwa ngozi, pamoja na kujamiiana. Watu walio na kesi mbaya zaidi wanaweza kupata vidonda kwenye uso, mikono, kifua na sehemu za siri.../

 

Tags