Serikali ya Sudan yapeleka msaada wa matibabu katika maeneo yenye vita
Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza kwamba imepeleka vifaa vya dharura vya matibabu katika mikoa iliyoathiriwa na mgogoro wa vita unaendelea hivi sasa nchini humo.
Kwa mujibu wa serikali ya Sudan, tani 250 za dawa muhimu, viuavijasumu na vifaa vya dharura vya matibabu vimepelekwa kwenye maeneo hayo.
Waziri wa Afya wa Sudan, Haitham Mohamed Ibrahim ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, msaada huo umetolewa ili kupunguza makali ya hali ya dharura ya kibinadamu baada ya Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kufanya uhalifu mkubwa katika vijiji zaidi ya 100 vya Jimbo la Gezira.
Amesema, hali ni mbaya sana katika mkoa wa Gezira kiasi kwamba imebidi hatua za dharura zichukuliwe ili kuwapunguzia mateso wakazi wa mkoa huo.
Mgogoro wa vita umeathiri mno huduma za afya nchini Sudan hasa katika maeneo yenye vita. Maduka mengi ya dawa mjini Khartoum yamefungwa kutokana na mapigano hayo na kusababisha uhaba wa dawa muhimu na kupaa vibaya bei zake.
Mripuko wa magonjwa kama vile kipindupindu, malaria, surua na homa ya dengue umezidisha maafa ya kiafya nchini humo. Wizara ya Afya ya Sudan inasema, zaidi ya kesi 28,000 za kipindupindu zimesharipotiwa na kwa uchache watu 800 wameshapoteza maisha kwa ugonjwa huo.
Vita baina ya majenerali wa kijeshii vilivyoanza mwezi Aprili 2023 vimeshapelekea watu 24,850 kuuawa na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao huko Sudan.