ICC yamhukumu miaka 10 jela mhalifu wa kivita kwa ukatili huko Mali
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imemhukumu kifungo cha miaka kumi jela mkuu wa polisi muasi kwa jinai za kivita na dhidi ya binadamu.
ICC imesema kuwa Al Hassan Ag Abdoulaziz AgMohamed Mahmoud aliye na umri wa miaka 47 alitenda uhalifu huo wakati mji wa Timbuktu huko Mali ulipokuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo magaidi.
Majaji wa ICC mwezi Juni mwaka huu walimtia hatiani Al Hassan Ag Abdoul Aziz Ag Mohamed Ag Mahmoud kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na utesaji alipokuwa mwanachama wa kundi la wanamgambo wenye misimamo ya kufurutu ada ambalo lilitwaa udhibiti wa Timbuktu kwa karibu mwaka mmoja tangu mwanzoni mwa mwaka 2012.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya ICC Kimberly Prost amesema kuwa hukumu waliyotoa inalingana na uzito wa uhalifu uliofanywa na hali ya mtu binafsi na hatia ya Bw Al Hassan.