Jul 26, 2016 16:54 UTC
  • 13 wauawa katika mashambulizi pacha ya mabomu Mogadishu, Somalia

Mashambulizi pacha ya mabomu yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 13 karibu na kambi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM na nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa katika mji mkuu Mogadishu.

Duru za polisi nchini humo zimeripoti kuwa, 7 miongoni mwa waliouawa katika hujuma hizo za kigaidi zilizofanyika karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege mjini Mogadushu ni maafisa usalama. Hata hivyo vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, 9 miongoni mwa waliouawa ni askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na watatu ni wanajeshi wa AMISOM.

Bishaar Abdi Gedi, ofisa wa polisi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika amesema vyombo vya usalama vimefanikiwa kuwaangamiza wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab ambao wametangaza kuhusika na mashambulizi hayo. 

Athari za shambulio la kigaidi Mogadishu, Somalia

Haya yanajiri siku tatu baada ya jeshi la Somalia kwa kushirikiana na askari wa AMISOM, kuanzisha operesheni kali ya kuwanasa wanachama wa al-Shabab katika eneo la Jubba, kusini mwa nchi ambapo wanamgambo kadhaa waliuawa.

Wanachama wa al-Shabaab waliotangaza utiifu wao kwa Daesh

Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabab wamekuwa wakiwalenga askari wa serikali na wale wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika na kadhalika viongozi wa serikali wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Kundi hilo ambalo limeshatangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh, linakusudia kuiondoa madarakani serikali ya Mogadishu na kuunda utawala wake.

Tags