Jul 27, 2016 07:22 UTC
  • Rais wa ICC atakiwa kujiuzulu kwa kupokea rushwa ili 'kumshtaki al-Bashir'

Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC anakabiliwa na mashinikizo ya kila upande ya kutaka ajiuzulu ili kupisha uchunguzi huru wa madai ya ufisadi wa kifedha dhidi yake katika kesi dhidi ya Rais wa Sudan Omar al-Bashir.

Gazeti la London Evening Post la Uingereza limeripoti kuwa, Rais wa ICC Silvia Alejandra Fernández de Gurmendi anatuhumiwa kupokea mamilioni ya dola za Marekani ili kuwahonga mashahidi bandia katika kesi dhidi ya Rais wa Sudan. Imearifiwa kuwa, Jaji Fernández de Gurmendi wa ICC alipokea jumla ya dola milioni 17 za Marekani kati ya mwaka 2004 na 2015 kutoka mashirika kadhaa yakiwemo Barting Holding Ltd, Atlantic Corporation, Genesis International Holdings na Napex International wakati ICC ilikuwa inafanya uchunguzi dhidi ya Bashir. Gazeti hilo limeandika kuwa, fedha hizo zilitumwa katika akaunti za makundi ya waasi kama vile Sudan Liberation Movement ambayo awali ilifahamika kama Darfur Liberation Front 2002.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan alipokuwa Uganda kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais Yoweri Museveni

Mashinikizo ya kujiuzulu Rais wa ICC yanajiri katika hali ambayo, Rwanda hivi karibuni ilipuuzilia mbali wito wa kumkamata Rais al-Bashir na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC alipozuru nchi hiyo kwa ajili ya kushiriki mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika mjini Kigali. Louis Mushikiwabo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda alisema nchi hiyo mbali na kuwa sio mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni ICC, lakini ilikataa kumkamata Rais wa Sudan kwa madai kuwa, mahakama hiyo 'imegubikwa na siasa' na kwamba imekuwa ikitumika kuwaandama viongozi wa bara la Afrika tu. Uganda, Kenya na Afrika Kusini ni baadhi ya nchi za Kiafrika ambazo zilikataa mwito wa ICC wa kumkamata kiongozi huyo alipozitembelea nchi hizo.

Viongozi wa AU mjini Kigali Rwanda.

ICC ilitoa waranti wa kumkamata Rais al Bashir mwaka 2009 na mwaka 2010, kwa tuhuma za makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliotokea mkoani Darfur, magharibi mwa Sudan.

Tags