Abuja yaijia juu Canada kwa kumyima 'viza' Mkuu wa Jeshi la Nigeria
Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Nigeria, Jenerali Christopher Musa, ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya ubalozi wa Canada katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, kumnyima yeye na maafisa wengine wakuu wa kijeshi viza ya kwenda Canada kuhudhuria hafla ya michezo ya maveterani wa vita huko Vancouver.
Jenerali Musa amesema kwamba, ingawa kutoruhusiwa kuingia Canada "kunavunja moyo sana," lakini kitendo hicho kinapasa kutuzindua Wanigeria kwamba, tunafaa "kusimama imara kama taifa na kukataa kutwezwa."
Michezo ya Vancouver Whistler 2025 ya kuwaenzi maveterani wa vita ilianza Februari 8, na inatazamiwa kumalizika kesho Jumamosi.
Akihutubia Mkutano wa Chama cha Kitaifa cha Taasisi ya Mafunzo ya Usalama huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria, Jenerali Musa amebainisha kuwa, “Tulitakiwa kuwepo huko Vancouver hivi sasa. Kwa kweli, nusu ya timu yangu tayari wamekwenda, lakini kwa bahati mbaya, ubalozi wa Canada, kwa sababu wanazozijua wenyewe, walitunyima viza.”
Kadhalika Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Abuja, Nuhu Ribadu, ameikosoa vikali serikali ya Canada kwa kuwanyimwa viza makamanda hao wa ngazi za juu wa jeshi la Nigeria na kueleza kwamba, "wanaweza kwenda kuzimu."
Akihutubia mkutano huo wa usalama mjini Abuja jana Alhamisi, Ribadu amesema, "Ingawaje inauma na hatua hiyo si ya heshima, lakini tuna amani, tuna nguvu, na ninakubaliana na wewe (Jenerali Musa) kwamba, huu ni wakati wa kurekebisha nchi yetu. Hii ni sababu nyingine ya kutulazimisha tufanye kazi kwa bidii ili kuifanya Nigeria iwe imara.”