Mapigano makali yaripotiwa kandokando ya ikulu ya rais mjini Khartoum, Sudan
(last modified Sun, 02 Mar 2025 07:15:31 GMT )
Mar 02, 2025 07:15 UTC
  • Mapigano makali yaripotiwa kandokando ya ikulu ya rais mjini Khartoum, Sudan

Baadhi ya vyanzo vya ndani vimeripoti kuwa Jeshi la Sudan limefanya mashambulizi makali dhidi ya ngome za wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) mjini Khartoum na kwamba mapigano makali yanashuhudiwa karibu na ikulu ya rais.

Vyanzo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa Jeshi la Sudan linashambulia kwa mizinga maeneo ya wapiganaji wa kundi la waasi la RSF mjini Khartoum, eneo la Nile Mashariki, na kaskazini mwa mji wa Al-Abidj, huku mapigano yakipamba moto karibu na ikulu ya rais mjini Khartoum.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Sudan imesema: Vikosi maalumu vya Jeshi la Taifa vinashambulia kambi za RSF kwenye maeneo kadhaa, kama Mtaa wa Al-Safaha Zalat, Kituo cha Al-Ghali, Hospitali ya Al-Jawda, na Shule ya Al-Nama kusini mwa mji mkuu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa vikosi vya jeshi vimeua wanamgambo kadhaa wa RSF na kukamata silaha zao katika operesheni hiyo.

Sambamba na hayo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesitisha usambazaji wa chakula cha msaada katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam nchini Sudan kutokana na kushtadi mapigano kati ya jeshi la serikali na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Awali, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk alionya juu ya hatari ya kuongezeka zaidi kwa vita nchini Sudan na kusema kwamba, kuna hatari kubwa ya kutokea vifo kutokana na njaa kwa kiwango cha kuogofya.

Tangu kuzuka vita vya ndani huko Sudan mwaka 2023 kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, karibu watu milioni 8.8 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi hiyo huku milioni 3.5 wakikimbilia nchi jirani.