Ripoti: Askari walioua Waislamu Nigeria washtakiwe
Jopo la uchunguzi lililotwika jukumu la kuchunguza mauaji ya Waislamu kaskazini mwa Nigeria limekiri kuwa jeshi la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika liliuawa Waislamu zaidi ya 300 katika mji wa Zaria jimbo la Kaduna.
Jopo hilo limethibitisha uchunguzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lililosema kuwa Waislamu karibu 350 wa madhehebu ya Shia waliuwa na askari wa Nigeria katika mji wa Zaria. Jopo hilo la majaji limependekeza kufunguliwa mashtaka wanajeshi waliouhusika na mauaji hayo ya kikatili mwishoni mwa mwaka jana.
Mwezi Aprili mwaka huu, Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International lilitangaza kuwa, jeshi la Nigeria liliua zaidi ya Waislamu 350 wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky mwezi Disemba mwaka jana.
Itakumbukwa kuwa tarehe 14 Disemba mwaka jana 2015, siku moja baada ya jeshi la Nigeria kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya Waislamu katika mji wa Zaria, liliizika miili ya wahanga hao katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo.
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria hata hivyo linashilikilia kuwa karibu watu 1000 waliuliwa na jeshi la nchi hiyo katika hujuma hiyo.