Diop: Ukraine inachochea ukosefu wa utulivu barani Afrika
(last modified Tue, 08 Apr 2025 06:41:20 GMT )
Apr 08, 2025 06:41 UTC
  • Diop: Ukraine inachochea ukosefu wa utulivu barani Afrika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop amesema Ukraine inavuruga utulivu barani Afrika kwa kuunga mkono makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel barani humo.

Katika mahojiano na shirika la habari la RIA Novosti jana Jumatatu, Diop amesema kuwa, hatua za Ukraine ni tishio kubwa kwa usalama wa kikanda.

"Lazima niseme kwamba Mali, ambayo pia imekata uhusiano na Ukraine, inaitazama Ukraine kama taifa la kigaidi, kwa kuwa Ukraine imetoa wito kwa uwazi na kutangaza uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi katika Sahel," waziri huyo amesema.

"Hii imesababisha vifo vya wanajeshi na raia wengi wa Mali," ameongeza mwanadiplomasia huyo mkuu wa Mali huku akisisitiza kuwa: Bamako inalaani vitendo vya Kiev, ni lazima iwajibike.

Diop pia amesisitiza kuwa, Mali na washirika wake wa kikanda wanaunga mkono juhudi za kutatua mzozo kati ya Moscow na Kiev, huku akisisitiza kwamba suluhisho lolote lazima lishughulikie masuala ya usalama ya Russia.

Alkhamisii iliyopita, Diop, alisema kuwa Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) ulioundwa na Mali, Niger na Burkina Faso mwaka 2023, umebadili kabisa mlingano wa nguvu za kimkakati kwa madola ya kikoloni ambayo yanataka kuendelea kutawala nchi hizo.

Alisema, "Napenda kukumbusha dhamira yetu ya pamoja ya kuongeza juhudi za kupambana na ugaidi…pamoja na wale wanaofadhili ugaidi, kama vile Ukraine."