Aug 03, 2016 03:57 UTC
  • 42 wauawa na kujeruhiwa katika shambulizi la bomu Libya

Makumi ya watu wameuawa na kujeruhiwa katika shambulizi la bomu la kutegwa garini lililolenga wanajeshi wa serikali katika mji wa Benghazi, mashariki mwa Libya.

Duru za kiusalama na hospitali zimearifu kuwa, watu 22 wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa baada ya gari lililokuwa na mabomu kulenga mkusanyiko wa askari wa jeshi la serikali linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar, katika wilaya ya Guwarsha. Habari zaidi zinasema kuwa, mkusanyiko huo wa askari wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ulikuwa unafanya mazungumzo katika eneo la makazi ya raia katika mji wa Benghazi, ambao umekuwa uwanja wa makabiliano kati ya vikosi vya serikali na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kwa muda wa miaka miwili sasa.

Benghazi umekuwa mji wa makabiliano kati ya Daesh na askari wa serikali kwa miaka 2 sasa

Shambulizi hilo linajiri mwezi mmoja baada ya askari 12 wa jeshi la Libya kuuawa katika shambulizi jingine la bomu la kutegwa garini katika mji huo wa Benghazi.

Aidha Ijumaa iliyopita, mapigano mapya baina ya askari wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na genge la kigaidi la Daesh yalisababisha mauaji ya askari watano wa serikali na wengine 28 kupata majeraha mabaya karibu na eneo la Dolar, yapata kilomita 1.5 kusini magharibi mwa mji wa Sirte.

Genge la kigaidi la Daesh nchini Libya

Wanamgambo wa Daesh wanatumia washambuliaji wa kujitoa muhanga, magari yaliyotegwa mabomu pamoja na mabomu ya ardhi kupunguza kasi ya kusonga mbele vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.

Tags