Shambulio jingine la droni laripotiwa Port Sudan, pande hasimu zinaendelea kupigana
Watu walioshuhudia jana Jumatano waliripoti kujiri shambulio jingine la ndege zisizo na rubani katika mji wa mashariki wa Sudan wa Port Sudan huku mapigano makali yakiendelea kati ya Jeshi la Taifa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Milio ya milipuko ilisikika karibu na kambi ya wanamaji ya Flamingo katika mji wa Port Sudan na mashuhuda wanasema Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Sudan kimezuia shambulio hilo.
Juzi Jumanne pia moto ulishuhudiwa huko Port Sudan baada ya shambulio la droni kuripotiwa katika maeneo kadhaa ya mji huo likiwemo maghala ya mafuta. Jeshi la Sudan limesema wanamgambo wa RSF wamehusika wa hujuma hiyo.
Mji huo ulioko katika Bahari Nyekundu umekuwa ukitumiwa kama mji mkuu wa utawala wa muda wa Sudan kufuatia kuzuka kwa mapigano ya ndani tangu Aprili 2023.
Maafisa wa serikali ya Sudan kwa mara nyingine tena wanalituhumu kundi la waasi la RSF kuwa linafanya mashambulizi ya droni dhidi ya miundombinu ya raia vikiwemo vituo vya umeme na taasisi nyingine katika mji wa kusini ya Merowe, Dongola, Dabba na Atbara.
Wanamgambo wa RSF wanapigana dhidi ya jeshi la Sudan katika vita vya kuwania madaraka ambavyo hadi sasa vimesababisha kuuawa maelfu ya watu na kuibua majanga mabaya zaidi ya binadamu.