Askari walioshirikiana na al-Qaeda Kodivaa wafungwa miaka 10 jela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12679-askari_walioshirikiana_na_al_qaeda_kodivaa_wafungwa_miaka_10_jela
Askari wawili wa Ivory Coast wamehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kushirikiana na kuwa na mafungumano na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Qaeda.
(last modified 2025-11-16T06:33:27+00:00 )
Aug 05, 2016 13:46 UTC
  • Askari walioshirikiana na al-Qaeda Kodivaa wafungwa miaka 10 jela

Askari wawili wa Ivory Coast wamehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kushirikiana na kuwa na mafungumano na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Qaeda.

Wawili hao wanatuhumiwa kuficha habari za kupangwa shambulizi la kigaidi la mwezi Machi mwaka huu mjini Abidjan, ambapo idadi kubwa ya watu waliuawa.

Kanali Ange Kessi, afisa wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo amesema wanajeshi hao waliokamatwa mwezi Julai mwaka huu walikosa kupiga ripoti kwa wakubwa zao licha ya kuwa na taarifa kuwa wanamgambo wa al-Qaeda walikuwa wanapanga shambulizi hilo.

Wanajeshi wakielekea Abidjan baada ya hoteli ya Grand Bassam kutekwa nyara na magaidi Machi 2016

Itakumbukwa kuwa, mwezi Machi mwaka huu watu 16 wakiwemo raia 14 na askari wawili waliuawa baada ya watu sita wenye silaha kushambulia hoteli za ufukweni katika eneo la Grand Bassam lililoko kilomita zipatazo 40 mashariki mwa mji mkuu wa kibiashara wa Ivory Coast, Abidjan.

Magaidi wa al-Qaeda nchini Kodivaa

Kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika eneo la kaskazini mwa Afrika (AQIM) lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na shambulio hilo. Shambulio hilo ni la tatu kubwa kufanywa na wanamgambo wa kundi hilo katika eneo la magharibi mwa Afrika tangu mwezi Novemba, ingawa ni la kwanza nchini Ivory Coast likitanguliwa na mashambulizi yaliyofanywa katika nchi za Mali na Burkina Faso.