11 wauawa na kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi Misri
Watu wanne wameuawa na wengine saba kujeruhiwa katika hujuma inayoaminika kuwa ya ulipizaji kisasi katika Peninsula ya Sinai nchini Misri.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, shambulizi hilo la kigaidi limefanyika usiku wa kuamkia leo katika mji wa el-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini.
Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi walitega mada za miripuko kwa ajili ya kuwaua maafisa wa usalama lakini mripuko huo umeua na kujeruhi raia. Hakuna kundi lolote la kigaidi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo.
Mapema jana Sheikh Ali Gomaa, Mufti Mkuu wa zamani wa Misri aliponea chupuchupu katika jaribio la mauaji baada ya watu wawili waliokuwa juu ya pikipiki kumfyatulia risasi alipokuwa akielekea msikitini mjini Cairo. Mufti huyo aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, Uwahabbi na Usalafi hauna chochote isipokuwa ni ugaidi na misimamo ya kufurutu ada.
Jaribio hilo la mauaji dhidi ya mwanachuoni huyo wa Misri limejiri siku moja baada ya jeshi la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kutangaza kuwa limemuangamiza kamanda mkuu wa kundi la kigaidi la Daesh katika Peninsula ya Sinai. Abu Duaa al-Ansari aliuawa pamoja na makumi ya wanachama wa kundi hilo la kitakfiri katika mashambulizi ya anga ya jeshi la Misri katika eneo la Sinai.